Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
KATIKA juhudi za serikali kuimarisha ubora wa elimu nchini, wazazi na walezi wametakiwa kuongeza ushiriki wao katika kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni kupitia mahudhurio ya vikao vya shule na ushirikiano wa karibu na walimu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alipokuwa akizungumza na wazazi na wanafunzi katika shule ya sekondari ya Zawadi iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mafanikio ya mwanafunzi yanahitaji ushirikiano wa serikali, jamii, wazazi na wanafunzi wenyewe.

Amesema serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza walimu pamoja na kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Mpogolo amesema pamoja na juhudi hizo, bado mwitikio wa baadhi ya wazazi katika vikao vya shule umekuwa mdogo jambo ambalo linaathiri ufuatiliaji wa maendeleo ya kitaaluma na kitabia vya watoto wao.

“Naomba wazazi washiriki vikao vya shule sambamba na kushirikiana na walimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kuongeza kiwango cha taaluma na ufaulu shuleni,” amesema Mpogolo.
Aidha, amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakituma ndugu au wafanyakazi wa nyumbani kuhudhuria vikao vya shule kwa niaba yao, hali inayopunguza mawasiliano muhimu kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi.

Amesema wanafunzi nao wanapaswa kuzingatia nidhamu, maadili mema na kuongeza bidii katika masomo ili juhudi zinazowekwa na serikali pamoja na wazazi ziweze kuleta matokeo chanya katika elimu.
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ushiriki wa wazazi na jamii katika maendeleo ya elimu ni miongoni mwa misingi muhimu ya kuongeza ubora wa elimu nchini, huku wataalamu wa elimu wakieleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya shule na wazazi husaidia kuongeza ufaulu, nidhamu na mahudhurio ya wanafunzi mashuleni.


More Stories
Wizara,TPSF kuongeza ushiriki kongamano la kiswahili
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini