
Na Israel Mwaisaka ,Rukwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Afraha Hassan, kwa niaba ya wananchi wa Wilaya hiyo, amepokea rasmi boti ya huduma za chanjo katika hafla iliyofanyika katika Halmashauri ya Kibiti, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza mara baada ya kupokea boti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Afraha Hassan, amebainisha kuwa uwepo wa boti hiyo utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za chanjo, hususan katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika na yale yenye changamoto ya miundombinu ya usafiri.
Aidha, alisema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa kuwafikia walengwa, wakiwemo watoto na wananchi waishio katika maeneo ya mbali, ili kuhakikisha wanapata huduma za chanjo kwa wakati.
“Kupatikana kwa chombo hiki kutaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za chanjo, hasa kwa watoto wanaoishi katika maeneo ya mbali,” alisema Hassan.
Alidai kuwa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya ili kuhakikisha boti hiyo inatumika kwa ufanisi na kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za kinga na kupunguza magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Hafla ya makabidhiano hayo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa, wataalamu wa afya pamoja na wadau wa maendeleo, ambapo walisisitiza umuhimu wa matumizi ya usafiri salama na wa uhakika katika kuboresha huduma za afya.

More Stories
Wajumbe wa Bodi ya REA waipongeza ETDCO
Bodi ya REA yaridhishwa na kasi ya usambazaji umeme Mbeya
Zingatia mtandao wa viwango wazinduliwa rasmi