April 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mawaziri washuhudia makubaliano ya fursa mpya za biashara, uwekezaji

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati zimefunguliwa kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Maelewano (MoU) kati ya Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) na National Export Promotion Council of Belarus.

Hafla iliyoshuhudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

Makubaliano hayo yanafungua milango ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zenye mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi, ikiwemo kilimo, viwanda na usindikaji, biashara ya bidhaa na huduma, teknolojia, madini, nishati, vifaa tiba, usafirishaji pamoja na upanuzi wa masoko ya kimataifa kwa bidhaa za Tanzania na Belarus.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kombo amesema ushirikiano huo unaweka msingi imara wa kupanua mahusiano ya kiuchumi yenye manufaa kwa mataifa yote mawili na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya biashara na uwekezaji.

“Makubaliano haya yanaweka msingi imara wa kufungua fursa mpya za ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili,” amesema Balozi Kombo.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov, amesema Belarus iko tayari kuendeleza ushirikiano wa vitendo utakaozalisha matokeo chanya ya kiuchumi na kibiashara kwa pande zote mbili.

“Tuko tayari kuendeleza ushirikiano wa vitendo utakaoleta matokeo chanya kwa mataifa yetu,” amesema Ryzhenkov.

Akizungumzia umuhimu wa makubaliano hayo kwa sekta binafsi, Rais wa TNCC, Vicent Minja, amesema MoU hiyo ni daraja muhimu la kufungua biashara na uwekezaji zaidi, akisisitiza utekelezaji madhubuti wa makubaliano hayo ili kuleta matokeo halisi.

“Sasa tunahitaji kuhamisha makubaliano haya kutoka kwenye nyaraka kwenda kwenye utekelezaji wenye matokeo,” amesema Minja.

Kupitia MoU hiyo, Tanzania na Belarus zinatarajiwa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kuongeza ubadilishanaji wa teknolojia na maarifa, kuchochea miradi ya pamoja, na kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia masoko mapya na fursa za kimataifa.