April 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji kwa wavulana kujenga uanaume imara

Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza

IMEELEZWA kuwa kadri miaka inavyozidi kwenda ndivyo wanaume wanavyokuwa hatarini kutokana na mambo mbalimbali yanayoendelea nchini hapa na duniani yanayolenga kufifisha uanaume.

Katika kukabiliana na hali hiyo taasisi ya Men at Work Global,imeweka mkakati wa miaka 10 ijayo ya kujenga kituo maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watoto na vijana wa kiume Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza Aprili 26,2026 Rais na Mwanzilishi wa taasisi ya Men at Work Global, Maxwell Shing’oma,katika kongamano la wanaume(men summit 2026), lililofanyika jijini Mwanza,amesema changamoto zinazowakabili wanaume kwa sasa zinatokana na mtindo wa maisha na jinsi mambo yalivyo,wengi wamekata tamaa,wamevunjika moyo,hawana ari na morari ya maisha.

Hivyo baadhi yao wakipata changamoto kidogo kwenye familia au wakiona maisha yamekuwa magumu kidogo yupo tayari kuondoka au kufanya vitu vya ajabu,kwa sababu anaona ni njia rahisi ya kupata umaarufu au kipato.

Maxwell amesema,ili kuondoa changamoto hiyo katika jamii ni muhimu kama nchi na wanaume,kuwekeza kwenye maarifa na malezi ya watoto wa kiume ili kuwe na familia na taifa bora.

Amesema,wanataka kituo hicho kiwe cha mfano ili kusaidia na kuinua hali ya watoto wa kiume kujitambua,kwa sababu ili upate wanaume walio bora ni lazima kuwe na wavulana waliopitishwa kwenye mchakato wa kuwaandaa.

“Tunataka shule zikifungwa nchi nzima watoto wa kiume wawe kwenye hicho kituo kwa ajili ya kuwajengea uwezo kimwili, kisaikolojia na kihisia.Hivyo tunaomba Serikali itusaidie tupate eneo kwa ajili ya kujenga kituo hicho,”amesema Maxwell.

Mshauri wa Maendeleo Binafsi,Timoth Kyara, amewasisitiza wanaume kuwa wasafi,kuzingatia utafutaji wa fedha salama huku wakilinda afya zao kwa kuhakikisha wanapata muda wa kupumzika.

“Fedha inahitaji mifumo haiji kwa maombi kwa kuwekewa mikono.Katika mchakato wa kutafuta fedha tunza afya yako,kula vizuri,lala vizuri katika saa 24 tumia saa 8 kupumzika kwa kulala,katika siku 7 za wiki siku moja pumzika na kwa mwaka mzima kwa wiki tatu hadi nne pumzika,”amesema Kyara.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Nchi, PLO Lumunia Foundation Tanzania,Joram Nkumbi,amesema mwanaume haonewi huruma bali anaitwa moyo huku akiwasisitiza wanaume kufanya kazi kwa uaminifu na bila janja janja.

“Ukiona mwanaume unahurumiwa yatakupata matatizo,tufanye kazi kwa bidii,usiwe mjanja mjanja,jenga usiku imara kwa kuwa mkweli.Mwanaume mzuri anajifunza kwa mwananume aliyemtangulia,”amesema Nkumbi.

Kwa upande wake Chifu Aron Mikomangwa,amewahimiza wanaume wasiwe watu wa kulalamika bali wanapaswa kulisimamia, kusimamia maamuzi,mpambanaji, mpiganaji na hawapaswi kuwa wana lia lia.