April 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pre-Betika Tulia Marathon kuwainua kiuchumi vijana Mbeya

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya

KUELEKEA mashindano ya Pre-Betika Tulia Marathon yatakayofanyika Mei 15 hadi 16 mwaka huu, Serikali imewataka wadhamini kuhakikisha wanatenga na kuandaa mabanda ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa katika viwanja vya Sokoine, jijini Mbeya, ili kuongeza ushiriki na kunufaisha wananchi kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 25, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Mohamed Azizi , kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, wakati wa ufunguzi wa mbio za Pre-Betika Mbeya Tulia Marathon 2026, ikiwa ni maandalizi ya mashindano makubwa yatakayofanyika katika Uwanja wa Sokoine.

Azizi amesema kuwa mashindano hayo ni fursa muhimu kwa vijana na wananchi kujikwamua kiuchumi, akisisitiza kuwa wengi wao wanaweza kutumia tukio hilo kufanya biashara mbalimbali na kujipatia kipato.

“Kwa asilimia kubwa washiriki ni vijana hii ni fursa yao kujiongezea kipato. Msikubali kuitwa hamna shughuli kupitia marathon hii, mnaweza kufanya biashara na kubadilisha maisha yenu,” amesema Azizi

Ameongeza kuwa maandalizi ya mabanda ya biashara yanapaswa kufanyika mapema, ndani na maeneo mengine na nje ya uwanja, ili kuruhusu wafanyabiashara wengi kushiriki kikamilifu wakati wa mashindano hayo.

Aidha, Azizi amesema tukio hilo pia litasaidia kuitangaza Mbeya kwa kuonesha vivutio vyake vya utalii, huku akibainisha kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za Taasisi ya Tulia Trust katika kuandaa mashindano hayo.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuwashirikisha wadau wa ajira na mafunzo ya ujuzi, akieleza kuwa vijana wengi bado wana mtazamo wa kutegemea ajira za serikali pekee, ilhali kuna fursa nyingi za kujiajiri.

“Ajira si lazima iwe serikalini. Kujiajiri ni njia muhimu ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesisitiza.

Vilevile, amewahimiza wananchi wa Mbeya kushiriki mashindano hayo kwa amani na nidhamu, akibainisha kuwa mkoa huo unatarajia kupokea wageni wengi wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Michezo kutoka Taasisi ya Tulia Trust, Lugano Mwangosi, amesema kuwa mbio hizo zinafanyika kwa mara ya kumi na zimekuwa chanzo cha fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa Mbeya.

Amesema uwepo wa washiriki wa kimataifa kutoka nchi kama Kenya na Uganda unaongeza thamani ya mashindano hayo, huku Mbunge wa Jimbo la Uyole akitarajiwa kutoa zawadi nono kwa washindi.

Mwangosi ameongeza kuwa fedha zitakazokusanywa kupitia mashindano hayo zitatumika kuboresha sekta za afya na elimu mkoani Mbeya, pamoja na kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.

Mbio hizo pia zitaambatana na michezo mbalimbali ya kijamii kama kukimbia kwenye magunia na mashindano ya kubeba yai kwenye kijiko, ambayo nayo hutoa fursa kwa washindi kushiriki katika marathon kuu.

Afisa Michezo wa Mkoa wa Mbeya,Robert Mfugale amesema Taasisi ya Tulia Trust imekuwa mstari wa mbele kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na kuwapatia huduma za afya wananchi wasiojiweza, ikiwemo bima ya afya na ujenzi wa makazi.

Amehitimisha kwa kusema kuwa mashindano hayo yamekuwa yakitangaza Mbeya kimataifa, na yana uwezo wa kukua zaidi na kuwa mbio za kimataifa zitakazovutia washiriki kutoka mataifa mengi zaidi.