April 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo, azindua kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”

Na Joyce Kasiki,Dodoma


WAZIRI wa Kilimo, Daniel Chongolo, amezindua rasmi kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” yenye lengo la kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na usimamizi bora ndani ya vyama vya ushirika nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Chongolo alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya ushirika, bado kuna changamoto katika kulinda rasilimali na mapato ya wanachama. Alipongeza juhudi zinazofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kusimamia na kuendeleza ushirika.
“Moja ya maeneo yanayotusumbua ni kulinda kile kinachoingia na kilichopo ndani ya vyama vya ushirika. Lazima tukubaliane kuwa tuna taasisi za usimamizi, lakini bado kuna haja ya kuimarisha ulinzi wa mali za wanachama,” alisema Chongolo.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya uwajibikaji, akifananisha na kazi inayofanywa na TAKUKURU, akisema sekta ya ushirika inayozungusha takribani trilioni sita za fedha haiwezi kuachwa bila ulinzi maalum.
Aidha, Waziri huyo alikosoa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanaofanya kazi kwa mazoea bila kuzingatia thamani ya mali za wanachama, akisisitiza kuwa nidhamu ya kifedha bado ni changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa kwa dhati.
Kwa upande wake, Msajili na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, alisema kampeni hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na kufanyiwa tathmini kila mwaka ili kupima mafanikio na kubaini changamoto.
Alieleza kuwa kampeni hiyo itajikita katika matumizi ya mifumo ya kidijitali, ukaguzi wa mara kwa mara, na kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kukiuka taratibu. Pia kutakuwa na mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa wadau na watoa taarifa (whistleblowers), pamoja na kuanzishwa kwa maafisa uadilifu ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
Dkt. Ndiege aliongeza kuwa lengo kuu ni kupunguza ubadhirifu, kuongeza uaminifu na kuhakikisha vyama vya ushirika vinawanufaisha wanachama wake kwa ufanisi zaidi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna changamoto kadhaa, ikiwemo baadhi ya vyama kutoa taarifa zisizo sahihi licha ya kuwepo kwa mifumo ya utoaji taarifa za kila mwezi na robo mwaka, hasa kwa vyama vya akiba na mikopo. Aidha, ripoti za COASCO zimeonyesha kuwepo kwa udhaifu katika ukaguzi, huku si vyama vyote vinavyokaguliwa kwa wakati kutokana na vikwazo vya rasilimali.
Alitaja pia ucheleweshaji wa mashauri yanayowasilishwa katika taasisi kama TAKUKURU na mahakamani, hali inayowaathiri wanachama wanaopoteza fedha zao na kuchelewa kupata haki.
Kwa ujumla, kampeni hiyo inalenga kuimarisha ushiriki wa wanachama, kuongeza matumizi ya teknolojia, kuimarisha ukaguzi, kutoa mafunzo ya uadilifu, na kushirikiana kwa karibu na taasisi za kisheria ili kuhakikisha nidhamu na uwajibikaji vinaongezeka.
“Tutahakikisha tunapunguza ubadhirifu na kuongeza uaminifu kwenye vyama vya ushirika. Wale wachache watakaokiuka taratibu, hatua kali zitachukuliwa mara moja,” alisisitiza.