Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma




WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amezindua Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi, akiwahimiza waajiri nchini kushirikiana na vijana watakaonufaika na mpango huo unaotekelezwa na VETA.
Akizungumza jijini Dodoma baada ya uzinduzi huo, Prof. Mkenda amesema kuwa programu hiyo inafadhiliwa kikamilifu na Serikali, hivyo hakuna fundi atakayelazimika kulipia gharama yoyote ili kushiriki.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo lazima uzingatie haki na uwazi, na kuagiza VETA kuhakikisha unawafikia walengwa wote bila ubaguzi.
Aidha, amebainisha kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na marejeo yake ya mwaka 2023, ambayo yanatilia mkazo elimu ya ufundi stadi katika kukuza ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa juhudi hizo zinaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26), unaolenga kuimarisha rasilimali watu na kukuza uchumi wa viwanda wenye ushindani, ili kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na tija.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Amir, amesema programu hiyo imekuja kwa wakati mwafaka, ikilenga kuongeza ushindani wa ujuzi na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo zabuni.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ameeleza kuwa jumla ya wananchi 14,400 wanatarajiwa kunufaika katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hiyo.
Baadhi ya wanufaika wamepongeza mpango huo, wakisema unawajengea kujiamini na kuwapa fursa ya kupata ajira na zabuni kubwa ambazo hapo awali walishindwa kutokana na kukosa uthibitisho rasmi wa ujuzi wao.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT