Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Benki ya I&M imeendelea kupanua uwekezaji wake katika sekta ya fedha nchini Tanzania kwa kufungua rasmi tawi lake la tisa katika eneo la Palm Village, Mikocheni jijini Dar es Salaam, hatua inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi na kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wateja wa rejareja pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Upanuzi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa benki hiyo kukuza shughuli zake nchini, ukiakisi imani yake katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania pamoja na ongezeko la mahitaji ya huduma za kifedha zilizo rafiki na nafuu katika maeneo ya mijini na vituo vinavyoibukia vya biashara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank, Zahid Mustafa, amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya muda mrefu ya benki kuendelea kuwekeza nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi, akisisitiza kuwa Tanzania ni soko muhimu kwa benki hiyo.
“Tanzania ni soko muhimu kwetu, na tunaendelea kujizatiti kuwekeza katika suluhisho bunifu pamoja na kupanua huduma zetu ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya wateja wetu,” amesema Mustafa.

Ameongeza kuwa benki hiyo inalenga kujenga mfumo imara wa huduma za kifedha unaowajumuisha watu binafsi, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na makampuni makubwa, ili kuhakikisha kila kundi linapata huduma stahiki kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za Rejareja na Kidijitali, Simon Gachahi, amesema ufunguzi wa tawi hilo unaashiria hatua mpya ya ukuaji wa benki hiyo inayochochewa na ubunifu wa huduma na upanuzi wa miundombinu ya utoaji huduma.

“Hii ni hatua muhimu kwetu na kwa wateja wetu, ikionesha dhamira ya kuwasogezea wananchi huduma za kifedha na kuunga mkono shughuli za kiuchumi katika ngazi zote,” amesema Gachahi.
Amesema benki inapanga kuongeza idadi ya matawi hadi kufikia 18 ndani ya miaka mitatu ijayo, huku ikiendelea kutoa bidhaa nafuu ikiwemo miamala ya bure kutoka benki kwenda simu pamoja na mikopo ya ununuzi wa mali yenye riba ya asilimia 9 ili kusaidia kukuza biashara na uwekezaji.

Aidha, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika huduma za kidigitali ikiwemo benki kupitia WhatsApp pamoja na ushirikiano na Airtel kupitia huduma ya “Kamilisha”, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa mikopo kwa Watanzania wengi zaidi hususan wanawake na vijana na hivyo kuchochea uchumi jumuishi.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati