Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru Arusha,Dkt. Alex Ernest amesema, watumishi zaidi ya 10 wa sekta ya afya katika Hospitali hiyo wamechukuliwa hatua za kinidhamu kati yamwaka 2024 na 2025.
Kati ya watumishi hao wapo madaktari Bingwa wawili na wauguzi sita, kufuatia ukiukwaji wa maadili ya kazi na kushindwa kuzingatia taratibu za utoaji huduma.
Akizungumza hayo juzi jijini Mkoani Arusha,Dkt.Ernest wakati akiongea na waandishi wa habari alisema alisema hospitali imejiwekea utaratibu wa kuripoti matukio kuanzia kwenye jamii yenyewe.
Akitolea mfano Dkt.Ernest amesema iwapo mtumishi wa afya anakiuka haki za mgonjwa basi yamewekwa mazingira ya wagonjwa kutoa taarifa.
“Tunachukua hatua, hatufanyi kwa kukomoa,tunafanya kwa kuhakikisha kwamba, kama watumishi wa serikali, kama watumishi wa afya, tunafuata kanuni na maadili ya kazi’ hasa katika sekta hii ya mama na mtoto” amesema
“Tunatoa elimu kwa watumishi juu ya namna bora ya kuwahudumia wagonjwa, ikiwamo lugha, mapokezi yenyewe na kuhakikisha mama anapata huduma eneo safi, ambalo halitakuwa hatarishi kwa afya yake.

Dkt. Alex amesema serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye eneo la rasilimali watu, hasa kwenye eneo la mama na mtoto.
“Kama hospitali kwa sasa tumetoka kwenye Madaktari bingwa watatu hadi madaktari bingwa 7, na kwa Watoto tuna madaktari bingwa 6.
“Kwa ujumla tuna madaktari bingwa 13 kwenye eneo la mama na mtoto”amesema
Amesema kufanya hivyo kumeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, wagonjwa kuhudumiwa kwa wakati na wataalamu wenye ujuzi katika maeneo hayo.
“Serikali imewekeza zaidi kwenye eneo la vifaa tiba, Rais Samia Suluhu, katika hili hatumdai, kwani aliwekeza zaidi kwenye vifaa tiba hasa vifaa vya uchunguzi vya kisasa, kama ultrasound, ili kutambua vihatarishi vinavyoweza kusababisha afya ya mama na mtoto”amesema
Dkt. Ernest amesema, bajeti ya dawa imeongezwa kwa kiwango kikubwa na serikali kuu, kama hospitali inapata asilimia 100 ya dawa zinazohusu magonjwa ya wanawake na Watoto.
Takwimu za Wizara ya Afya Tanzania zinaonyesha kuwa, Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto inaendelea kuwa suala la kipaumbele katika ngazi ya kimataifa na kitaifa.
Viongozi wa dunia walipitisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) mwaka 2015, ambapo lengo la tatu linataka kupunguza viwango vya vifo vya kinamama, hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000, na kwa Watoto malengo ya SDG yanataka kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1,000.
Kwa mujibu wa Utafiti Wa Demographia na Afya wa Tanzania (TDHS) mpaka sasa vifo vya kinamama vimepungua kutoka, 556 katika kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016/17 mpaka vifo 104 katika kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022/23.
Kupungua kwa vifo hivi ndiko kulikochagiza kutunukiwa kwa tuzo ya Kinara wa Afya ya Mama na Mtoto kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika, Addis Ababa Ethiopia.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati