Na Martha Fatael, TimesMajira Online
WAANDISHI wa habari wamehimizwa kuchukua nafasi yao kikamilifu katika kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi, badala ya kusubiri majanga kama mafuriko ndipo wayazungumzie.
Wito huo umetolewa Machi 24, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mdahalo wa wadau wa habari kuhusu namna bora ya kuripoti masuala ya tabianchi. Mdahalo huo uliandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na taasisi ya Wajibika.

Mhariri wa Mafunzo na Mawasiliano kutoka Shirika la Thomson Foundation (TF), Catherine Mackie, amesema vyombo vya habari vinapaswa kuandika kwa mtazamo unaojenga na unaowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mackie anaeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni jambo linaloendelea sasa, hivyo ni muhimu kwa vyombo vya habari kuhakikisha sauti za wadau mbalimbali zinasikika kupitia taarifa wanazozalisha.

Aidha, anasisitiza kuwa hakuna ulazima wa kuwa na dawati maalum la mazingira ndani ya vyombo vya habari kwani kila mwandishi ana wajibu wa kuripoti masuala ya mazingira kwa weledi na ubunifu.
Mkurugenzi wa Programu kutoka taasisi ya Wajibika, Adelaide Addo-Fenng, anatoa muhtasari wa mradi wa uandishi wa habari za mabadiliko ya tabianchi akieleza kuwa unalenga kuwajengea uwezo waandishi ili kuboresha namna wanavyoripoti masuala hayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya mfuko wa maendeleo ya vyombo vya habari Tanzania (TMF), Dastan Kamanzi, anasisitiza umuhimu wa kuendeleza miradi ya uandishi wa habari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzingatia ubora wa maudhui yanayolenga kuelimisha jamii.

Akifunga mdahalo huo, Mkurugenzi wa Nchi kutoka taasisi ya Oxford Policy Management (OPM), Dkt. Charles Soke, anawahimiza waandishi wa habari kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha kazi zao za kila siku.

Huku mwandishi Said Machiel akisema mradi huo umemsaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa na uwezo wake katika kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi.






More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini