Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Serikali imeendelea kuboresha bandari zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo za Ziwa Victoria na Tanganyika ili kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa njia ya bandari.
Hayo yameelezwa Machi 22, 2026 mkoani mwanza, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya utendaji wa serikali katika sekta ya uchukuzi.
Msigwa amesema,Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko inajengwa kwa fedha za ndani shilingi bilioni 280, hadi kufikia Machi 21,2026, ujenzi wake umefikia asilimia 95 na ukikamilika unatarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa.
“Serikali imeendelea kuboresha bandari zilizopo Ziwa Victoria ili kuchochea biashara na nchi jirani. Hadi Februari 2026, mradi wa uboreshaji wa bandari ya Bukoba na Kemondo umekamilika na uboreshaji bandari ya Mwanza Kaskazini umefikia asilimia 75,”amesema Msigwa.
Amesema, Serikali imeendelea kuboresha bandari zilizopo Ziwa Tanganyika ikiwemo bandari ya Kigoma kwa fedha za Japan ambapo hadi kufikia Februari, 2026, ujenzi umefikia asilimia 9.0 na ujenzi wa ofisi za TPA katika bandari za Ziwa Tanganyika umekamilika.
Pia amesema, Serikali imeendelea kuboresha bandari zilizopo Ziwa Nyasa ikiwemo ya Mbamba Bay kwa gharama ya shilingi bilioni 75.85. Hadi kufikia Februari 2025, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 47.
Huku ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 39.21 umekamilika,Serikali ilitoa maeneo kwa ajili ya kuhudumia shehena ya nchi zingine ambapo nchi hizo kwa sasa zimeanza uendelezaji wa maeneo hayo.
“Shirika la Reli Tanzania(TRC), inaendelea na hatua za awali za maandalizi ya kuunganisha reli ya SGR na Bandari Kavu ya Kwala na kuwa na stesheni ya SGR katika eneo hilo,”amesema Msigwa.
Aidha Msigwa,amesema,Serikali imeanza hatua za awali za kuanzisha bandari kavu katika Mkoa wa Morogoro itakayohudumia shehena ya mizigo inayosafirishwa kwa reli ya SGR kutoka Bandari ya Dar-es-Salaam, ili kupunguza msongamano wa malori katika mikoa ya Dar-es-Salaam, Pwani na Morogoro.
Sanjari na hayo Msigwa,amesema Serikali imeendelea na ujenzi wa kituo kikuu cha uratibu wa masuala ya utafutaji na uokozi katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 98.
Pia inaendelea na ujenzi wa vituo vidogo vitatu vya utafutaji na uokozi vinavyojengwa kwenye eneo la Geita, Ukerewe na Musoma ambapo utekelezaji wake katika eneo la Kanyara Geita umefikia asilimia 91, Ukerewe umefikia 85 na Musoma umefikia 91.
“Serikali imenunua boti maalum ya wagonjwa kwa ajili ya Ziwa Victoria, ambayo tayari imewasili na iko tayari kutoa huduma. Pia, imenunua boti moja ya utafutaji na uokoaji Ziwa Tanganyika, boti mbili Ziwa Victoria na boti moja Ukanda wa Bahari ya Hindi (Tanga),”amesema Msigwa.
Vilevile amesema Wizara hiyo inaendelea na ujenzi wa minara mitatu ya mawasiliano katika Ziwa Victoria, ambapo minara ya Kisiwa cha Soswa na Kunenge imefikia asilimia 50 na Kisiwa cha Kweru umefikia asilimia 70.

More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini