Na Mwandishi wetu ,Timesmajira Online, Mbeya
WAKATI Waislamu wakijiandaa kuelekea Sikukuu ya Idd, Spika Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, ametoa msaada wa futari kwa waumini 204 wasiojiweza kutoka misikiti 17 ya jimbo hilo.
Msaada huo ulikabidhiwa Machi 17, 2026 katika Msikiti wa Wilaya wa Uyole kupitia Taasisi ya Tulia Trust, ukiwalenga waumini wanaoishi katika mazingira magumu wakati huu wa mfungo wa Ramadhani.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja wa Taasisi hiyo, Jackline Boaz, amesema wamekabidhi mifuko 204 ya chakula kwa niaba ya mbunge huyo ambaye hakuwepo eneo la tukio.

Amesema kila msikiti ulipendekeza waumini 12 wenye uhitaji, na kila mfuko ulikuwa na mchele kilo tano, unga wa ngano kilo moja, sembe kilo moja, tende kilo moja pamoja na maharage kilo moja.
“Tumelenga kuwasaidia waumini hawa kupata futari katika kipindi hiki cha mfungo, lakini pia kuwapa nafuu wanapoelekea kusherehekea Sikukuu ya Idd,” amesema i
Boaz.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Mashekhe Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ibrahim Bombo, amempongeza Dkt. Tulia kwa moyo wa kujitolea, akisema amekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Mbeya kwa muda mrefu.
Amesema kila msikiti ulihusishwa katika zoezi hilo kwa kuleta orodha ya wahitaji, wakiwemo wazee na watu wenye kipato cha chini.

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Alhaji Msafiri Nyarambaha, amesema Dkt. Tulia ameendelea kuwa kinara wa utoaji wa futari mkoani humo, akisisitiza kuwa jitihada zake zimechangia kuimarisha mshikamano na amani baina ya jamii za dini mbalimbali.
“Matendo haya yamekuwa yakileta umoja mkubwa, hata kwa kushirikisha waumini wa dini tofauti katika futari, jambo linaloimarisha mshikamano wa kijamii,” amesema.
Ameongeza kuwa licha ya nafasi kubwa ya uongozi aliyonayo, Dkt. Tulia ameendelea kuwa karibu na wananchi na kuishi maisha ya kawaida, hali inayomfanya kukubalika zaidi miongoni mwa wakazi wa Uyole.

More Stories
China na Tanzania kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Madini na maendeleo ya jamii
TANESCO yazindua ndege nyuki kuboresha ukaguzi miundombinu ya umeme nchini
Serikali yaagiza taasisi za serikali,kuongeza kasi ya uhamasishaji wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia