Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Jumuiya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania(SAUT), Mwanza, wametakiwa kuzienzi tunu alizoziacha Hayati Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu.
Profesa Mahalu alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, alifariki Machi 9,2026,wakati akioatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI), jijini Dar-es-Salaam.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT,Askofu wa Jimbo Kuu la Geita,Flavian Kassala,Machi 11,2026,wakati akiongoza waombolezaji waliojitokeza katika siku maalumu ya SAUT ya misa ya kumuombea na kuomboleza kifo cha Balozi Profesa Mahalu,iliofanyika chuoni hapo,jijini Mwanza.
Askofu Kassala,amesema Balozi Profesa Mahalu,alijitoa kwa ajili ya kujihudumia binafsi na kuhudumia taasisi,huku akisisitiza kuwa tunu hizo zinazotakiwa kuenziwa alizoziacha ni pamoja na unyenyekevu,upendo,mshikamano, mila na desturi za asili pamoja na kuzungumza lugha asili bila kujali usomi wake.
“Chuo tumepata pengo kubwa, sifa yake hakuwa mchoyo, alizunguka sehemu mbalimbali kutafuta maarifa kwa ajili ya kuboresha chuo.Pia ameandaa matunda na ameyarithisha,kwa hiyo tuna matumaini makubwa kwani ameacha wale watakaofundisha yale waliyofundishwa,wakiyazingatia watafikia ngazi ya ubingwa wa sheria kama yeye,”amesema Askofu Kassala na kuongeza:
“Taasisi ya SAUT imepoteza baba mwema wa familia lakini pamoja na kutuacha,kuna urithi ametuachia na kuna wakati alikemea.Hakuchoka kutupenda,hakuchoka kututumikia, alituonesha tabasamu hata wakati anakwenda kuangalia afya yake,”.
Kwa mujibu wa Askofu Kasala,Profesa Mahalu alikuwa chachu ya kuongezeka kwa wanafunzi, kutafuta wahadhiri wabobezi,kuanzisha programu za masomo zinazopikwa kwa ajili ya chuo, aliheshimu mipaka yake, kwa maono yake alilihakikishia baraza la chuo na taasisi inaendelea kusonga mbele, hivyo urithi aliowaachia utakuwa tunu ya kuijenga SAUT.
“Hayo yote ni urithi ambayo tuyatumia yana mchango mkubwa, kama SAUT tunaamini falsafa yake ya unyenyekevu na upendo wake itatuongoza, hivyo tuendeleze unyenyekevu na mshikamano,”amesema.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo cha SAUT, aliitaka jumuiya ya wanafunzi, wahadhiri na menejimenti kuwa na haki ya kusonga mbele kwani wanayo mengi ya kujifunza huku sauti itabaki Profesa Mahalu itabaki kwao.
Amesisitiza kuwa Makamu Mkuu huyo wa Chuo (Profesa Mahalu) licha ya usomi wake hakusau mila na desturi, alipenda kuzungumza lugha ya asili ya Kisukuma hivyo tuenzi mila na desturi, vyetu viweze kutusindikiza.
Kaimu Makamu Mkuu wa chuo cha SAUT ,Profesa Juvenalis Asantemungu,amesema,” Tumepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa lakini tukitambua kuwa ni mapenzi ya Mungu yametimizwa.Huu ni msiba mkubwa siyo kwa familia tu bali kwa taifa kutokana na mchango wake,”.
Profesa Juvenalis,amesema Balozi Profesa Mahalu,aliondoka mapema mwaka jana, kwenda kuchunguzwa afya yake, hata alipokuwa Afrika Kusini aliendelea kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo ya chuo licha ya kuwa alikuwa anaumwa.
Ameeleza kuwa, Balozi Profesa Mahalu, alijiunga na chuo hicho mwaka 2013 kama Mwalimu Mwandamizi wa Sheria na mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa SAUT Mwanza.
“Ametuacha na maumivu makubwa pia urithi wa uongozi ndani ya chuo na nje ya chuo,ameacha alama kubwa na baada ya kuteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho alikuwa na kipaumbele kuhakikisha chuo hicho kinakuwa bora,”amesema Profesa Juvenalis.
Hivyo, chuo kitakumbuka juhudi zake za kuhakikisha mazingira ya chuo yanaboreshwa kwa wanafunzi na walimu,alijenga ujirani mwema kati ya chuo na taasisi.Pia alizunguka barani Afrika kuunganisha chuo hicho na taasisi mbalimbali duniani.

“Maono yake yalikuwa anaenzi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwamba chuo kikuu ni mahali pa kuleta fikra mpya,”amesema.
Amesema mazishi yatafanyika Machi 14,2026,katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, baada ya Misa Takatifu itakayofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Peter.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda, amesema,” Natoa pole kwa Kanisa Katoliki na jumuiya ya SAUT kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.Tumejifunza tabia njema ya upole,usikivu na unyenyekevu,tujaribu kutengeneza hadithi nzuri tukiwa duniani ili tukiondoka tusimuliwe vizuri,”alisema Mtanda.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi SAUTSO-Paul Kashinje, kwa niaba ya wanafunzi ameahidi kuwa wataenzi matendo ya unyenyekevu,moyo wa upendo,huruma na uchapakazi wa marehemu Profesa Mahalu,hakuwa na ubaguzi wowote na alijitoa kwa taasisi na taifa kwa ujumla.


More Stories
Mahundi azindua kamati kuwasaidia wenye uhitaji
TPDC:Serikali ipo hatua za mwisho majadiliano gesi asilia
Mahundi,Child Support watoa msaada shule Jumuishi