Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,-Bukoba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera imesaidia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 57.1 za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Wilaya ya Misenyi ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa TAKUKURU mkoani Kagera, Vangsada Mkalimoto, alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake.
Mkalimoto amesema fedha hizo zinatokana na makusanyo ya kodi pamoja na faini zilizotozwa kwa mizigo na magari yaliyokuwa yakiingizwa nchini kwa njia ya magendo kutoka Uganda bila kuwa na vibali halali.
Amefafanua kuwa TAKUKURU Misenyi kwa kushirikiana na kikosi kazi cha kuzuia magendo wilayani humo, mwezi Desemba 2025 ilifanikiwa kukamata magari matano, yakiwemo malori matatu na magari mawili ya abiria aina ya Hiace. Magari hayo yalivuka mpaka wa Tanzania na Uganda pamoja na vituo vya ukaguzi vya Kyaka bila kulipa kodi.
Magari hayo ni pamoja na lori lenye namba za usajili T 525 DNJP na tela namba T 811 DHA lililokuwa limebeba tani 38 za karanga kutoka Uganda, gari lenye namba T 509 EDN (Fuso Tandam) lililokuwa limebeba tani 16 na kilo 300 za karanga na maharage, lori lenye namba T 457 ELV na tela namba T 459 ELU lililokuwa limebeba tani 33 za karanga, gari la abiria aina ya Toyota Hiace lenye namba T 754 DJW lililokuwa limebeba injini ya gari pamoja na gari lenye namba T 435 DFJ lililokuwa limebeba katoni 303 za pombe haramu kutoka Uganda.
Amesema magari hayo yote yalibainika kuingiza bidhaa nchini bila kibali na bila kufuata taratibu za uingizaji wa bidhaa.
“Ili kuhakikisha Serikali inapata mapato yake ya kodi kama ilivyokusudiwa, TAKUKURU Misenyi kwa kushirikiana na kikosi kazi pamoja na TRA ilihakikisha wamiliki wa magari hayo wanalipa faini za magari, mizigo na tozo za serikali kupitia namba ya malipo(control number) walizopewa na TRA,” amesema Mkalimoto.
Aidha,amesema TAKUKURU itaendelea kuwafuatilia kwa karibu watumishi wa umma katika vituo vya ukaguzi watakaobainika kufumbia macho vitendo vya ukwepaji kodi.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria