Na Penina Malundo,Timesmajira
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa matangi 15 yakuhifadhia mafuta yenye thamani ya Sh Bilioni 678.6 ambapo ni sehemu ya utanuzi wa bandari wenye lengo la kuongeza ufanisi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amesema uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika eneo la Kigamboni Mnadani jijini Dar es Salaam Februari 4 mwaka huu
ambaye Dkt. Samia ataongoza tukio hilo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya Uchukuzi na Uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Amesema ujenzi wa matangi hayo unaonyesha dhamira ya kweli ya serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha mikakati ya kupanua miundombinu ya bandari nchini.
“Ujenzi wa matangi haya ni sehemu ya mkakati wakuongeza uwezo wa bandari unaoenda sambamba na na ujenzi wa magati ambapo kwa sasa tumeanza na Gati namba moja ikiwa ni sehemu ya mkakati ya kuongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam katika kuingiza shehena kubwa zaidi.

”Kila gati itakayojengwa itakuwa na urefu wa Kilomita 500 na uwezo wa kupokea meli mbili kwa wakati mmoja,kukamilika kwa mradi huu utakuwa na uwezo wa kupokea tani Milion 60 kwa mwaka na kufanya bandari yetu kuwa miongoni mwa bandari zenye ushindani mkubwa,”amesema.
Prof. Mbawara amesema katika kipindi cha Julai mpaka Disemba Mwaka jana,Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia taribani Shehena za mizigo tani Milioni 19.9 huku matarajio ya Serikali ni kufikia tani Milioni 40 mwisho wa mwaka 2025/26.

Amesema kiasi hicho cha ukuaji kimevuka malengo waliojiwekea jambo lilowalazimu kuendelea kupanua miundombinu ya bandari na kwendana na mahitaji ya soko.”Serikali inaendelea na ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhia mafuta yatakayoongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kwa mita za ujazo 378000 hatua hii itapunguza muda kwa meli za mafuta kukaa bandarini na kutoka kwa wastani wa siku 3 badala ya siku 10.
”Hali hii itaweza kuongeza ufanisi kuvutia wawekezaji zaidi na kuimarisha usalama wa nishati hiyo,”amesema

Aidha amesema maboresho hayo yanaenda na mkakati wa kuimarisha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kupitia Reli ya Mwendokasi (SGR) katika kuhakikisha kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mizigo yote inaenda kwenye mtandao wa reli kusafirishwa.
Amesema kwa sasa zaidi ya asilimia 90 ya mzigo unaotoka bandari ya Dar es Salaam inapitia barabarani hiyo maana yake ni kuwa barabara zinakufa,ajali zinakuwa nyingi,ucheleweshaji wa mizigo kutoka sehemu moja hadi nyingine na kusababisha msongamano.
”Mizigo ikipita kwenye treni hali itakuwa nzuri zaidi,Sekta ya uchukuzi imeendelea kuwa muhimili muhimu wa uchumi wa taifa kwa kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya mapato ya Serikali kupitia kodi ya Forodha pamoja na kuingiza wastani wa Dola za Marekani Milioni 2.48 kwa mwaka kama fedha za kigeni kutoka wizara za uchukuzi za nchi za jirani,”amesema.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama