March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFF yatinga na safu tatu mpya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Kahama

Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanyiwa marekebisho ya muundo kwa kuanzisha kurugenzi tatu mpya zitakazofanya kazi chini ya Rais wa shirikisho hilo, hatua inayolenga kuboresha utendaji na usimamizi wa soka nchini.

Akizungumza Februari 28,2026,baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa 20 wa TFF uliofanyika mjini Kahama, Rais wa TFF Wallace Karia,amesema marekebisho hayo yamekuja kufuatia haja ya kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa soka kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.

Kwa mujibu wa Karia, kurugenzi zilizoanzishwa ni pamoja na Kurugenzi ya Miundombinu ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia ujenzi, ukarabati na maendeleo ya miundombinu ya michezo nchini.

Kurugenzi ya pili ni ya Kusimamia Ligi itakayoshughulikia uendeshaji na usimamizi wa mashindano ya ligi mbalimbali chini ya TFF, huku Kurugenzi ya tatu ikiwa ni ya Manunuzi itakayoratibu masuala yote ya ununuzi kwa kuzingatia uwazi na taratibu za kifedha.

Karia amesema lengo kuu la marekebisho hayo ni kuongeza ufanisi, uwajibikaji na weledi katika kusimamia soka la Tanzania.

“Tunataka kuona mpira unasimamiwa kwa weledi,kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa,”amesema Rais wa TFF.

Katika hatua nyingine, Rais huyo amesisitiza kuwa kuanzia sasa Mwamuzi (Refa) yeyote atakayebainika kuvuruga mchezo kwa makusudi atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Ameonya kuwa endapo atapatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo jela, akisisitiza kuwa TFF haitavumilia vitendo vinavyoharibu taswira ya soka.

Kwa upande wake, mwenyeji wa mkutano mkuu huo wa 20, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya TFF, Azan Mufti,amesema kufanyika kwa mkutano huo Kahama kumeleta manufaa katika sekta ya michezo wilayani humo na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.


Mufti amesema,TFF imepitisha kuanzishwa kwa kituo cha michezo kitakachojengwa katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Barrick – Buzwagi, uliokuwa umefungwa, hatua itakayosaidia kukuza vipaji na kuinua michezo katika ukanda huo.

Pia amesema,kuna mpango wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu Wilaya ya Kahama utakaokuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 15,000.

Hata hivyo Mufti,amewahimiza wadau wa michezo Mkoa wa Shinyanga kuacha majungu, kushikamana na kufanya kazi kwa umoja ili kufanikisha maendeleo ya michezo na kuunga mkono juhudi za TFF katika kuimarisha soka nchini.