Na Joyce Kasiki, Dodoma
WATENDAJI wa serikali na wajumbe wa Kamati za kitaifa za utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili awamu ya pili (MTAKUWWA II 2024/25–2028/29) kwa wanawake na watoto kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana bado hayatoshi bila mifumo imara ya uwajibikaji kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, wakati wa uzinduzi wa vikundi kazi vya kamati ya Mpango huo ambao uliozinduliwa mwaka 2024 .
Alisema licha ya taarifa kuonyesha kama kuna kuoungua kwa vitendo vya ukatili lakini hali bado ni mbaya katika maeneo ya wananchi huku akisema anapokea jumbe nyingi kutoka kwa wananchi wakilalamikia mambo mengi yasiyofaa yanayifanyika vikiwemo vigodoro,vijamvi wakati kamati za MTAKUWWA zipo hadi katika ngazi ya kata.
“Kwa kuwa mtu ambaye hayuko ndani ya sekta hii anaweza kudhani ukatili umepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na taarifa zinazowasilishwa, lakini hali halisi bado ni mbaya,na hii ni kutokana na mapungufu katika utekelezaji wa shughuli hii ya utekelezaji wa Mpangonwetu huu.”alisema Dkt.Gwajima na kuongeza kuwa
“Nina miaka mitano ndani ya wizara hii, lakini najiuliza kwa nini mimi najulikana zaidi kuliko MTAKUWWA yenyewe? Kwa nini nipokee jumbe usiku na mchana kutoka kwa wananchi wakati kuna mifumo mpaka ngazi ya kata?” alihoji.
Waziri huyo alieleza kushangazwa na hali ya yeye kuonekana kama mhimili mkuu wa kupokea na kutatua malalamiko ya wananchi, badala ya watendaji waliopo kwenye idara na kamati husika kuchukua jukumu lao kikamilifu.
Alisisitiza kuwa MTAKUWWA ni mpango wa serikali, wenye bajeti na mikakati iliyopangwa, hivyo utekelezaji wake haupaswi kumtegemea mtu mmoja.
Akizungumzia eneo la uchumi wa kaya, ambalo ni miongoni mwa maeneo manane ya kipaumbele ya mpango huo, Dkt. Gwajima alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa vikundi kuhusu kukosa mikopo au kupewa fedha pungufu zinazoshindwa kukamilisha miradi yao.
Alitoa mfano wa ziara yake Ubungo, ambako alikuta vikundi vikilalamikia kucheleweshewa mikopo, lakini baada ya yeye kuagiza, fedha zilipatikana ndani ya miezi miwili.
“Kwa nini niseme ndipo vikundi vipate mikopo na kunishangilia mimi? Kamati za uchumi wa kaya zilikuwa wapi kubaini changamoto hizo mapema?” alihoji, akitaka tathmini ya kina kufanyika ili kubaini mapungufu ya kimfumo.
Katika eneo la mila na desturi, Waziri huyo alitaka kujua kama vitini na miongozo ya majadiliano ya kimila vinafanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Alieleza kusikitishwa na kuendelea kwa vitendo vya ukatili vinavyofanywa kwa kisingizio cha mila, huku vyombo vya dola na serikali za mitaa vikiwa karibu na matukio hayo bila kuchukua hatua.
Alisisitiza kuwa kamati zote kuanzia ngazi ya mtaa, kata, wilaya na mkoa zinapaswa kuhakikisha ajenda ya kupinga ukatili inajadiliwa mara kwa mara kama ilivyoelekezwa awali na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikaki za Mitaa (TAMISEMI).
Ameagiza kupata taarifa za kika robo mwaka ili kulinganisha yaliyoripotiwa na uhalisia wa wananchi.
Dkt. Gwajima pia alieleza wasiwasi wake juu ya mmomonyoko wa maadili, ongezeko la migogoro ya kifamilia na kuvunjika kwa ndoa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha malezi, msaada wa familia na maandalizi ya vijana wanaotarajia kuingia kwenye ndoa.
“Tunaozesha, lakini ndoa zinavunjika kwa kasi. Je, tunawapa vijana maarifa ya kutosha ya maisha ya ndoa?” alihoji.
Aidha, aligusia changamoto za usimamizi wa sheria na utoaji wa leseni za biashara katika maeneo ya makazi, akitolea mfano malalamiko aliyopokea kutoka Mkuranga kuhusu baa inayokesha na kusababisha usumbufu kwa jamii.
Alisema si jukumu lake kusimamia usajili wa biashara hizo moja kwa moja lakini yeye ndiye anapokea malalamiko hayo hali inayoonyesha namna gani ambavyo hakuna uwajibikaji wa kila mmoja katima eneo lake.
Kwa ujumla, Waziri huyo aliwataka wajumbe wa kamati na watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kujikita katika utekelezaji wa vitendo, ikiwemo kubaini mapengo ya kisera, kisheria na kimiongozo yanayokwamisha mapambano dhidi ya ukatili.
“Kazi kubwa mmeifanya, lakini jiandaeni kwa kazi kubwa zaidi,tuondoke kwenye vitabu, twende kwenye vitendo,kila mtoto alindwe, na kila mwanamke aishi katika mazingira salama,” alisisitiza.
Alisema,uzinduzi wa vikundi kazi vya MTAKUWWA II unalenga kuimarisha uratibu, uwajibikaji na ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha malengo ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto yanafikiwa ifikapo mwaka 2029 huku akisistiza wahusika lazima wawe wadadisi ili kuifikia jamii kwa malengo yaliyokusudiwa.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama