Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Watumiaji wa barabara mkoani Mwanza wakiwemo abiria,madereva na mawakala wa mabasi,wametakiwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Wito huo umetolewa Februari 28,2026,na Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA),Mkoa Mwanza,wakati wa zoezi la ufanyaji usafi pamoja na utoaji elimu ya usalama barabarani lililofanyika stendi ya kuu ya mabasi Nyegezi, wilayani Nyamagana mkoani humo.

Katibu wa RSA Mkoa wa Mwanza,Subira Sabi,amesema ni muhimu kufuata sheria za usalama barabarani, pamoja na kuzingatia utaratibu kuanzia hatua za kupanda gari hadi kushuka.
Ambapo amewahimiza abiria kuhakikisha wanakaa kwenye siti zilizo na mkanda huku akiwasisitiza umuhimu wa kufunga mikanda wawapo ndani ya vyombo vya usafiri.
Hivyo amewasisitiza kutosita kumuuliza kondakta au dereva endapo kama siti hazina mikanda au kama kuna changamoto yoyote ya kiusalama.
Sabi,amewasihi abiria kufanya matumizi sahihi ya tiketi za mtandao ili kuongeza uwazi na usalama kwa wasafiri.
“Baadhi ya abiria hawana uelewa kuhusu mfumo wa tiketi mtandao, huku baadhi ya mawakala wakishutumiwa kutoa tiketi zisizo rasmi badala ya kutumia mfumo wa kielektroniki kama inavyotakiwa,”amesema Sabi.
Kwa upande wake, Balozi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Nyamzala Nduttu,amewataka madereva kuzingatia mwendo salama na kuepuka uendeshaji wa kasi unaoweza kusababisha ajali.
“Usalama wa abiria unapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza wakati wote wa safari.Wamiliki wa mabasi wahakikishe magari yao yana mikanda ya usalama inayofanya kazi na kuwaelimisha abiria kuhusu umuhimu wa kuitumia,”amesema Nduttu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa RSA Mkoa wa Mwanza,Flora Kibage,amesema utoaji elimu ya usalama barabarani na ufanyaji usafi wa mazingira ni zoezi endelevu hivyo watakuwa wakifanya mara kwa mara.
Amesema elimu ya usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja abiria, madereva, mawakala na mamlaka husika ili kuhakikisha safari salama kwa wote.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama