March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LHRC,PALU waiomba serikali kurejea Mahakama ya Afrika

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Arusha.

SERIKALI imeombwa kurejea kuruhusu watu binafsi au Asasi za kiraia kuishitaki katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu (ACHPR) yenye makao makuu yake jijini Arusha,ili kukuza masuala ya haki za binaadamu na Diplomasia ya kimataifa .

Mwaka 2019 Serikali ya Tanzania ilijiondoa katika itifaki kifungu cha 34(6) kinacho ruhusu wananchi na Asasi za kiraia kuishitaki kwa kile ambacho ilielezwa ni baada ya kubainika kuwepo kwa dosari katika maamuzi ya mahakama hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kongamano la Wadau wa mahakama hiyo, ambalo linaendelea jijini Arusha,kabla ya kuanza vikao vya mahakama hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha sheria na Haki za Binaadamu(LHRC) Dkt.Wakili Anna Henga na Mtendaji Mkuu wa chama cha wanasheria wa Afrika(PALU), Wakili Donald Deya walisema haileti sura nzuri kimataifa kwa Tanzania kujiondoa kushitakiwa Arusha.

Amesema kwa kuwa sasa Serikali inajitahidi sana kurejesha diplomasia yake kimataifa ni wakati muafaka kurejea katika mahakama hiyo.

Dkt.Henga ambaye amekuwa mmoja wa wazungumzaji katika Kongamano hilo amesema , Tanzania licha ya kujitoa imekuwa ikitekeleza baadhi ya hukumu zilizotolewa na mahakama hiyo.

“Kuna maamuzi ya kesi ya uchaguzi yaliyotolewa na mahakama hiyo,kutaka wakurugenzi waondowe kusimamia uchaguzi serikali imetekeleza japo si kwa mambo yote lakini walau kuna hatua zimechukuliwa na kuondolewa wakurugenzi”amesema .

Amesema kwa sasa Watanzania wanaotaka kufungua kesi wanalazimika kupeleka kesi zao kwanza tume ya haki za binaadamu na watu Banjuu nchini Gambia na ndipo kesi iletwe.Arusha jambo ambalo wananchi wengi hawawezi.

Akiendesha mjadala kuhusu utelelezwaji wa maamuzi ya mahakama hiyo kwa nchi za Afrika Dkt. Henga alisema miaka 20 ya mahakama hiyo kuna maamuzi ambayo yametolewa na kutekelezwa na nchi 34 za Afrika ambazo ni wanachama wa mahakama hiyo.

Kwa upande wake,Wakili Deya amesema haoni sababu za msingi za Tanzania kuendelea kuzuia kushitakiwa kwani hoja kuwa maamuzi ya mahakama hiyo yalikuwa yakikiuka Katiba ya Tanzania sio sahihi.

“Maamuzi ya kesi nyingi yaliyotolewa hayatofautiani na maamuzi ya mahakama za ndani ya Tanzania na vyombo vingine vya umoja wa mataifa hivyo hakuna dosari”alisema

Hata hivyo Deya amesema wanaimani serikalo ya Rais Samia Suluhu itakamilisha mchakato wa kurejea katika mahakama hiyo hivi karibuni.

Deya ambaye ni mmoja wa mawakili wa kesi zaidi ya 20 ambazo zimefunguliwa katika mahakama hiyo na Watanzania, amesema kimsingi kesi nyingi ambazo zimefunguliwa ni za wafungwa ambao wanaamini hawakutendewa haki na mahakama za ndani Tanzania.

Wakili Deya amesema pia kesi nyingine ni za kisiasa ambazo, baadhi tayari zimetolewa maamuzi na serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya maboresho katika sheria zake.

Mahakama ya Afrika ya haki za binaadamu za watu, yenye makao.makuu yake jijini Arusha, ilianzishwa mwaka 2004 kutokana na maazimio ya Umoja wa nchi huru za Afrika mwaka 1998.