Mwandishi Wetu,Timesmajira Online- Bukoba,
Jumla ya Kaya 15,274 kutoka katika makundi maalum yasiyokuwa na uwezo yenye watu 67,718 kunufaika na mpango wa bima ya afya kwa wote mkoani Kagera baada ya Serikali kuwalipia kupitia ufadhili wa moja kwa moja kwa awamu ya kwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Kanali Yahya Kido, amesema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo (RCC),kilichofanyika mkoani humo.

Kanali Kido,amesema ili kumpunguzia mwananchi gharama za matibabu Januari 20 mwaka huu umezinduliwa mpango wa bima ya afya kwa wote, ili kufikia dhamira ya Serikali ya kila mwananchi kuwa na bima hiyo.
Amesema zoezi la uandikishaji wa kaya hizo unaendelea katika halmashauri zote mkoani humo hadi kufikia Februari 20,mwaka huu jumla ya Kaya 6,802 zenye wanufaika 18,965 tayari zimeandikishwa.
Amesema mkoa umeshafanya vikao mbalimbali na mafunzo kwa viongozi wa ngazi zote ili kuhakikisha kila mtu anakuwa na uelewa kuhusu bima ya afya kwa wote.
Hata hivyo ametoa maelekezo kwa wajumbe wote wa kikao hicho, kuhakikisha wanasimamia zoezi la uandikishaji bila vikwazo vyovyote na elimu iendelee kutolewa kwa wananchi.
Mariam Buberwa mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba,amesema wananchi walio wengi hawana elimu ya kutosha juu ya bima ya afya kwa wote.
Buberwa,amesema Serikali imefanya jambo zuri kuja na mpango huo kwa sababu magonjwa hayapigi hodi huja ghafla bila taarifa,unaweza kuugua bila kuwa na fedha hivyo kusababisha kukosa matibabu kwa wakati.
“Elimu itolewe kwa wananchi kuanzia vikao vya mitaa ili kuweza na uelewa wa kutosha na kuona umuhimu wa kuwa na bima ya afya katika familia zao,”amesema Buberwa.
Jackson Joackim,amesema Serikali iandae mpango maalum wa kutoa elimu ya bima hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kutoa fursa ya wananchi kuielewa zaidi.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina