March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPAA yaokoa bil.586.5

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma

MAMLAKA ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeokoa Shilingi bilioni 586.5 baada ya kuzuia utoaji wa tuzo za Zabuni 43 zilizokuwa zimetolewa kwa wazabuni waliokosa uwezo wa kifedha na sifa za kitaalamu za kutekeleza miradi husika.

Hayo yamesemwa Jijini hapa leo Februari 25,2026 na Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha Uongozi wa Awamu ya sita ambapo amesema kupitia kitengo cha rufaa, Mamlaka imesajili mashauri 196 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma. Kati ya mashauri hayo, zabuni 43 zenye thamani ya Shilingi bilioni 586.5 zimezuiwa kutolewa kutokana na wazabuni husika kutokidhi vigezo vya kifedha na kitaalamu.

“Serikali ya Awamu ya Sita inaamini kuwa usuluhishi wa migogoro hauwezi kufanikishwa katika mazingira ya ubaguzi wala pale ambapo fursa na haki za kiuchumi na kiraia hazitolewi kwa usawa. Kwa hivyo, hatua ya Mamlaka ya Rufani kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuji 43 waliokosa sifa za kutekeleza zabuni, inaimarisha mchakato wa usuluhishi wa migogoro – moja ya falsafa nne,”amesema Sando.

Hata hivyo Sando amesema katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika sekta ya ununuzi wa umma, Mamlaka imekamilisha moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST).

Amesema kuwa moduli hiyo imerahisisha usajili na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa, na kuongeza uwazi katika mchakato wa ununuzi wa umma.

“Tangu kuanza kutumika kwake, jumla ya malalamiko 549 yamewasilishwa na kushughulikiwa na taasisi nunuzi, huku rufaa 26 zikiwasilishwa na kuamuliwa na Mamlaka ya Rufani kupitia mfumo huo,”amesema.

Aidha, amesema katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuwawezesha vijana na makundi maalum, PPAA imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana 878 katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ili waweze kushiriki kikamilifu na kudai haki zao katika michakato ya ununuzi wa Umma.