Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Geita
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imesaini mkataba wa ubia na kampuni ya Plantcor Mining and Plant Hire (Pty) Ltd kwa ajili ya kuendeleza leseni saba za utafiti na uchimbaji madini ya dhahabu katika eneo la Kigosi, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.
Huku katika utekelezaji wa mradi huo wanapaswa kupanua wigo wa utafiti wa madini ili kusaidia na kuwanufaisha wachimbaji wadogo wa eneo hilo na kurudisha kwa jamii.

Akizungumza Februari 24,2026 katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo,Naibu Waziri wa Madini,Dkt.Steven Kiruswa, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kupanua uwekezaji kwenye sekta ya madini na kuendeleza rasilimali za taifa kwa manufaa ya Watanzania.
Alisema,mradi utatekelezwa kwa mfumo wa ubia ambapo STAMICO itakuwa mbia kwa niaba ya Serikali huku Plantcor wakichangia mtaji, teknolojia, mitambo na utaalamu wa kiufundi katika hatua za utafiti wa kina, uendelezaji na uzalishaji.
“Mradi utakapoanza uzalishaji na kutoa faida suala la kurudisha kwenye jamii(CSR),lizingatiwe hasa kufungua miundombinu ya barabara,kujenga shule,hospitali au vitu vingine ambavyo wananchi watataka,”alisema Dkt.Steven.
Pia aliwasisitiza wananchi kuheshimu mipaka itakayowekwa katika eneo la mradi huo,wasivamie badala yake waache muwekezaji afanye uwekezaji bila bugudha huku wakitumia fursa hiyo kufanya uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya uchimbaji madini ya Plantcor, Josef Wilmans,alisema kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika uchimbaji madini, utoaji wa huduma za mitambo na usimamizi wa miradi ya madini barani Afrika.
“Tunafanya shughuli katika mnyororo mzima wa sekta ya madini kuanzia uchimbaji mpaka kuingiza dhahabu sokoni.Tutaleta utaalamu wa kiufundi, teknolojia,utafiti pia kwa wachimbaji wadogo na fedha(mitaji),”alisema Wilmans na kuongeza:
“Tutazalisha ajira kwa watanzania na kuongeza thamani katika madini yatakayochimbwa na kunufaisha jamii yote inayozunguka mradi na taifa kwa ujumla.Tutafanya kazi kwa kuzingatia kiwango kinachokubalika pamoja na kulinda mazingira,”.
Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya uchimbaji ya Plantcor nchini Tanzania,Deogratius Kumalija,alisema Serikali imeweka mazingira ambayo yanawavutia wawekezaji kutoka nje kufanya uwekezaji nchini hapa.
“Katika mgodi huu tunategemea kuwa na ajira 20,000,ambazo ni za wazawa ikiwemo Ushirombo na maeneo mengine yanayozunguka eneo la mradi na ni watanzania.Wawekezaji hawa watakuja wachache kwa ajili ya kufanya kazi za kitaalamu,kiuchumi na uendeshaji kwa kutumia teknolojia yao,”alisema Kumalija.
Kumalija alisema,kupitia kanuni za ushiriki wa wazawa(Local content regulations), kutakuwa na biashara ambazo ni kwa ajili ya kusambaza malighafi na huduma nyingine ambazo zitahitajika katika uendeshaji wa mradi huo.
Alisema,nchi inapata faida inapopata wawekezaji kupitia kodi,mchango kwenye uchumi kwa sababu ukiangalia muundo wa ubia katika mikataba hiyo unakuta pia serikali inakuwa na asilimia yake.
“Katika uwekezaji huu STAMICO itakuwa na asilimia yao kama taasisi inayofanya biashara kwenye sekta ya madini,pia kuna asilimia 16 ambayo kisheria lazima ilipwe kwa ‘Treger Register ‘(TR).Yote haya yanaongeza ukusanyaji wa mapato ya nchi na uchumi unaanza kwenda juu,”alisema Kumalija.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO,Dkt.Venance Mwase, alisema shirika hilo litaendelea kuwa lango la uwekezaji katika sekta ya madini nchini hapa.
Dkt.Mwase,alisema kupitia STAMICO, uwekezaji huo utaleta mabadiliko kiuchumi na katika maisha ya watu wa Ushirombo na jamii inayozunguka mradi huo pia watanufaika.
“Mradi huu unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja katika hatua za utafiti, ujenzi na uzalishaji, pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja kupitia sekta za usafirishaji, chakula, malazi na huduma nyingine za kijamii. Serikali itanufaika kupitia mapato ya kodi kwa mujibu wa Sheria ya Madini na tozo nyingine za kisheria,”alisema Dkt.Mwase.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi STAMICO,Simon Sirro,alisema katika utekelezaji wa mradi huo atahakikisha uwazi na uwajibikaji unazingatiwa,maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla yanazingatiwa,mradi kufikia hatua ya uzalishaji kwa wakati na ufanisi pamoja na kusimamia sheria,kanuni na taratibu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita,Martine Shigela,alisema matarajio yao kupitia uwekezaji huo ni ajira kuongezeka na huduma zote zipatikane ndani ya Bukombe na Mkoa huo huku akiwahimiza wananchi kuchangamkia fursa ya kufanya uwekezaji katika sekta mbalimbali kupitia mradi huo.
“Kwa ujumla,wananchi changamkieni fursa hii ili muweze kujiona kiuchumi, kama hauwezi kuchimba madini,uza chakula, mbogamboga,fuga kuku na mambo mengine ili fursa hizi zibakie hapa kwetu na kutunufaisha,”alisema Shigela.




More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina