Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Shinyanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana,Dkt. Joel Nanauka, amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili vijana na kuhakikisha fursa za kiuchumi zinazotolewa zinawafikia kwa wakati na kwa ufanisi.
Dkt.Nanauka amesema hayo Februari 21,2026,wakati akizindua Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga,ambapo amewataka vijana kuweka mbele uzalendo, nidhamu na ubunifu ili waweze kunufaika na rasilimali na fursa zilizopo.

Amesisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wa vijana katika maendeleo ya Taifa, hivyo itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Vijana mnapaswa kuwa na ndoto ya kesho iliyo bora kiuchumi. Maisha hayana huruma, hivyo jengeni nidhamu ya kutumia muda wenu vizuri na kujiwekea malengo yanayotekelezeka,”amesema Dkt.Nanauka.
Aidha,amewataka vijana kuwa na mtazamo chanya na wenye mafanikio katika kuzitazama fursa zinazotolewa na Serikali huku akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji maandalizi, juhudi na uthubutu.
“Fursa zipo, lakini ili ufanikiwe ni lazima ujipange na kujiandaa. Serikali itaendelea kuwaunga mkono, lakini jukumu la msingi liko mikononi mwenu,”amesema.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliohudhuria uzinduzi huo wameeleza kuwa jukwaa hilo litakuwa chachu ya kuwapa maarifa, mitandao na mbinu za kutumia fursa za kiuchumi kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.




More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina