Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana, imekabidhi mkopo wa vifaa vyenye thamani ya sh.milioni 200 kwa vikundi viwili vya vijana mkoani Mwanza,vyenye jumla ya wakikundi 39,baada ya maandiko miradi yao ya biashara ya ufugaji na usafirishaji kukidhi vigezo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt.Joel Nanauka, alikabidhi vifaa hivyo Februari 19,2026, kwa vikundi hivyo vinavyojishughulisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba pamoja na usafirishaji wa mizigo,baada ya kuzindua Jukwaa la Vijana Mkoa wa Mwanza.

Amesema vikundi hivyo ni miongoni mwa vilivyowasilisha mawazo ya biashara baada ya kongamano la vijana lililofanyika Desemba 2025, jijini Mwanza, likishirikisha vijana na wahitimu wa elimu ya juu zaidi ya 600.
“Leo tumewaletea sh. milioni 200 kwa vikundi viwili, Kitwima Youth Group cha Wilaya ya Nyamagana,kinachoendesha mradi wa ufugaji wa kisasa wa samaki,kinapata vifaa vyenye thamani ya milioni 100 ikiwemo vizimba sita,vifaranga 60,000, chakula cha samaki na vifaa vyote vinavyohitajika.Pia kikundi cha waendesha bajaji za mizigo cha Buswelu, Wilaya ya Ilemela kimekopeshwa bajaji 12 za zenye thamani ya milioni 100,”amesema Dkt.Nanauka.
Dkt.Nanauka amesema kuwa, dhamira ni kuona miradi hiyo inasimamiwa vizuri pia, fursa hizo ni chache kati ya nyingi zinazotengenezwa na serikali, inafanya hivyo ili kuwaonesha vijana kuwa huo si mwisho, waendelee kuwasilisha maandiko yao.
Amesema kuwa Mkoa wa Mwanza una fursa nyingi za kiuchumi kutokana na rasilimali zilizopo ikiwemo sekta ya uchumi wa bluu inayochangia asilimia 70 ya uzalishaji wa samaki, huku hekta 140,000 zikifaa kwa kilimo cha bustani.
Pia sekta za viwanda vya uchakataji na usindikaji wa vyakula, ngozi, bidhaa za chuma, uvuvi kama ajira za kuongeza thamani mazao, uchimbaji wa madini na uchakataji wa mazao ya mifugo.
“Mwanza ni kitovu cha biashara ,una fursa katika huduma za bandari, ufugaji, utalii na teknolojia.Kuna fursa za kilimo,madini, ufugaji na uvuvi ambazo zinaweza kuwapa vijana fursa ya kujiajiri na kuajiri,” amesema Dkt.Nanauka.
Pia amesema lengo la Serikali ni kuona vijana wanatoka kuwa wasambazaji wa bidhaa na kuwa wazalishaji kwa kumiliki viwanda vya kuongeza thamani na waweze kuajiri wengine.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa viongozi kuwa na uwazi na kuhakikisha vijana wanapata taarifa kuhusu fedha za mikopo zinazotolewa kwa kundi hilo na kusiwe na upendeleo, ambapo wizara hiyo ina falsafa tatu za kwenda kwa kasi, kuondoa vikwazo na kuwezesha vijana kupata fedha.
Amesema kufanya hivyo kutaifanya Wizara hiyo kufikika na akawaelekeza vijana kuwa wizarani hapo wao siyo mabosi bali ni watumishi wa vijana,pia wanajitahidi kutumia teknolojia.

“Ili kufanikisha falsafa hiyo tumeanzisha dawati la kituo cha huduma (call center)ili kupata msaada au fursa zinazopatikana na jukwaa linalenga kufikia vijana wengi zaidi.Juhudi hizi zote zinafanywa na Serikali ili kuondoa changamoto ambazo zimetajwa na vijana na Rais alitaka tufanye changamoto za vijana kuwa fursa,”amesema Dkt. Nanauka
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Waendsha Bajaji za Mizigo na Pickup,Buswelu wilayani Ilemela,Wilbert Malale,amedema, mkopo huo wa bajaji 12, kutoka serikali utapanua wigo wa mradi wa kikundi na kufanya kiwe na bajaji 19,awali walipata mkopo wa bajaji 7 kutoka halmashauri.
“Tupo wanakikundi 32, matarajio yetu ni Kila mwanakikundi kumiliki bajaji yake ili tukue zaidi na kuweza kumiliki magari.Mkopo unaotolewa na serikali unatupa unafuu, ukichukua bajaji kwa mtu binafsi kwa wiki unarejesha sh. 120,000 ila huu unarejesha sh. 70,000,hivyo kufanya uchumi kuimarika,”amesema Malale.
Mwenyekiti wa kikundi cha Kitwima Youth group,Suzana Sayi,amesema, kikundi chao chenye wanachama saba kati yao wakike watatu,matarajio baada ya kumaliza kurejesha mkopo wa vifaa waliopewa na serikali ni kila mmoja atakuwa na kizimba chake cha kufugia na hivyo kujikwamua kiuchumi.
“Kulingana na uchumi wa buluu kwa sasa ufugaji wa samaki unakwenda kwa kasi,ni biashara inayolipa ikifanywa kwa malengo.Tumeona vijana wengi wamefanikiwa na sisi tunataka tufanikiwe,”amesema Sayi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kafiti Kafiti,amesema,Rais Samia amewaamini vijana na kusikia kilio chao na kuanzisha Wizara ya Vijana ambapo zaidi ya asilimia 60 ni vijana na ndio nguvu kazi ya taifa,hivyo lazima kuwe na hali ya kujenga taifa.
“Serikali lazima iande mazingira mazuri na miundombinu wezeshi kwa vijana, kujiajiri kwani haiwezi kuajiri wote.Katika utekekalezaji wa Dira ya 2050, lazima serikali kuandaa mpango wa kuwezesha vijana wetu, hivyo lazima ije na mkakati ili kujua kila kada inayomaliza elimu kwa kiwango cha elimu inakwenda wapi,”amesema Kafiti.
Ameshauri kuwa ni wakati sasa wa kuimarisha sekta ya kilimo kwa vijana ambao wanatoka JKT waende kulima, kwani kilimo ndio uti wa mgongo huku akiziomba taasisi za sekta za kifedha kupunguza masharti ya utoaji mikopo kwa vijana ili waweze kujiajiri na kujiwezesha kiuchumi.

.Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi,amesema, Mkoa wa Mwanza, ni wa pili kuwa na idadi kubwa ya watu ikikadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 3.6 huku vijana umri kati ya miaka 15-35, wakiwa ni zaidi milioni 1. 4 sawa na asilimia 39.4.
Amesema takwimu za mwaka 2024 mchango wa pato la taifa, Mwanza ilichangia asilimia 7.2 sawa na zaidi ya tirioni 14.8 huku uchumi wa mtu mmoja mmoja sawa na sh. milioni 3.7.
“Uchumi ukichangiwa na kilimo, mifugo,uvuvi,viwanda na ujenzi na mengineyo.Serikali kama itawekeza na kuwezesha vijana katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba,kuwakopesha vifaa tunaweza kuongoza katika uchangiaji wa pato la taifa na kuupita Mkoa wa Dar-es-Salaam kwani una fursa ya kuzungukwa na maji kwa asilimia kubwa,”amesema Makilagi.
Pia, mwaka 2021hadi 2026 Mkoa huo ulitenga jumla ya fedha bilioni 18.1, ambazo zilipelekwa kwenye vikundi vya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu.
“Bilioni 6.34, zimewanufaisha vijana 2401,wanawake bilioni 9.462,watu wenye ulemavu bilioni 2.3 huku zaidi ya bilioni 8.9, zikipelekwa kwa vijana, zaidi ya milioni 400 zimewezesha vijana zaidi ya 33 kupitia mradi wa BBT baada ya kufundishwa ufugaji na unenepeshaji ng’ombe,”amesema Makilagi.



More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina