Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA)imesema ili kukuza Ushiriki wa Wenye Mahitaji Maalum serikali inampango wa kuwezesha watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo wenye ulemavu kupata fursa zaidi za kujiunga na kujifunza ufundi stadi.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Februari 16,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana.

CPA Kasore amesema kuwa Serikali kupitia VETA inataka kuwezesha kundi hilo kupata ujuzi, kuajiriwa au kujiajiri, hivyo kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Afua mahsusi ambayo VETA imefanya mwaka huu ni kufadhili wanafunzi wote 195 wenye ulemavu waliodahiliwa katika vyuo vya VETA kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu. VETA itagharamia ada za mafunzo kwa miaka yote ya mafunzo, kuanzia Ngazi ya kwanza hadi ya Pili.
“Napenda kutumia fursa hii kuwahamasisha wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuwaleta watoto wao kwenye vyuo vyetu tushauriane ili nao wajiunge na mafunzo ya ufundi stadi, hivyo kupata ujuzi unaowawezesha kujikwamua kiuchumii na kimaisha kwa ujumla.
Vilevile CPA Kasore amesema kuwa Serikali imeelekeza nguvu mpya katika kuimarisha elimu ya ufundi stadi ili kuongeza ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
‎
Amesema chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, elimu ya amali imepewa kipaumbele maalum na kuhusishwa na miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa (SGR), maendeleo ya bandari, uchumi wa buluu, sekta ya madini na gesi.
‎Ameeleza kuwa kwa sasa VETA ina vyuo 80 vinavyohudumia zaidi ya wanafunzi 86,000 kwa mwaka, huku ujenzi wa vyuo vipya ukiendelea katika wilaya 64. Lengo ni kuongeza idadi ya vyuo hadi 152 ifikapo mwaka 2027 na kufikisha udahili wa wanafunzi 250,000 kwa mwaka.

‎Katika kuboresha upatikanaji wa mafunzo, amesema VETA imeondoa mtihani wa mchujo ili kutoa nafasi kwa waombaji wote wenye sifa kujiunga na mafunzo. Pia imeanzisha utaratibu wa mafunzo ya jioni kwa wanafunzi waliopo kazini au wenye majukumu mengine ya mchana.
‎Pia amesema wahitimu wa elimu ya juu wanaojiunga na kozi za ufundi stadi sasa wanaondolewa baadhi ya masomo waliyokwisha soma, hatua inayowawezesha kuhitimu kwa muda mfupi zaidi. Hatua hiyo imelenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi mahiri katika soko la ajira.
Hata hivyo ‎CPA Kasore amewahimiza vijana, wanawake na makundi maalum kuchangamkia fursa zilizopo VETA, akisisitiza kuwa ufundi stadi ni mhimili wa ajira, uzalishaji na maendeleo endelevu ya Tanzania.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina