Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewaomba Waislamu nchini kuiombea dua nchi ili matatizo yaliyopo yatatuliwe kwa njia ya amani, haki ipatikane kwa usalama, na kuepuka vitendo vya migogoro vinavyowanufaisha wachache wasioitakia mema Zanzibar.
Akizungumza baada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Iptisam, mkoa wa kusini Pemba Othman amesema kila Muislamu anayeitakia mema nchi anapaswa kuepuka kushabikia migogoro na badala yake kutumia nafasi yake kusuluhisha tofauti zilizopo.
“Kila Muislamu anayeitakia kheri nchi hii asishabikie watu kugombana; ni vyema kutumia nafasi yake kusuluhisha,” amesema.

Katika kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani, amewakumbusha waumini umuhimu wa kuhakikisha riziki wanazotafuta pamoja na vyakula wanavyofungulia swaumu vinapatikana kwa njia halali.
“Haiwezekani mtu achume haramu na ale haramu kisha aseme amefunga mwezi mtukufu wa Ramadhani,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Khatibu wa msikiti huo, Yusouf Mwalim Zubeiry, ameeleza kuwa uadilifu ni kutenda yaliyo sahihi kwa watu walio chini ya mamlaka ya mtu bila kufuata matamanio ya nafsi.
Aidha, ameonya kuwa Mwenyezi Mungu hayuko pamoja na wanaotenda kinyume na maadili mema na kwamba dhulma imeharamishwa kwa wanadamu wote.

Swala hiyo ilihitimishwa kwa dua maalum ya kuiombea kheri Zanzibar pamoja na wananchi wake.


More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani