Na Martha Fatael, TimesMajira Online
Licha ya Mlima Kilimanjaro kulindwa na sheria mbalimbali za mazingira, wataalamu wa uhifadhi, viongozi wa jamii na maofisa wa serikali wanasema changamoto kubwa si ukosefu wa sera au taasisi, bali kutokuwepo kwa uratibu wa kisheria na kiutendaji kati ya mamlaka zinazohusika moja kwa moja na usimamizi wa misitu na hifadhi zinazouzunguka mlima huo.
Kwa sasa, jukumu la uhifadhi limegawanywa kati ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA)kupitia Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) na serikali za mitaa, hali ambayo imeibua mgongano wa majukumu, uwajibikaji hafifu na kunufaika kidogo kwa jamii zinazozunguka rasilimali hizo.
Taasisi nyingi, lakini mfumo mmoja wa pamoja haupo
Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, kisheria serikali za mitaa zina wajibu wa kusimamia mazingira ndani ya maeneo yao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 (EMA). Hata hivyo, uhalisia unaonesha kuwa sehemu kubwa ya misitu inayozunguka Mlima Kilimanjaro haipo chini ya halmashauri, bali inasimamiwa na taasisi za serikali kuu.
Akizungumza katika kongamano la kitaifa la uhifadhi wa milima na vyanzo vya maji lililofanyika Arusha, mtaalamu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi Prof. Jamidu Katima aliwahi kueleza kuwa changamoto ya uhifadhi nchini haipo kwenye idadi ya taasisi, bali kwenye kukosekana kwa mfumo wa uratibu wa pamoja.
Kwa mujibu wa Prof. Katima, kila taasisi hufanya kazi chini ya sheria yake maalum, jambo linalosababisha uhifadhi kufanyika kwa vipande vipande badala ya kuzingatia ikolojia nzima ya mlima.
Serikali za mitaa kubaki pembeni
Katika warsha ya wakuu wa idara za mazingira za serikali za mitaa iliyofanyika Moshi, mtaalamu wa sera za mazingira Dkt. Venance Mayunga, alieleza kuwa licha ya EMA 2004 kuzipa halmashauri wajibu wa kisheria wa kusimamia mazingira, mamlaka yao huwa dhaifu pale misitu inapokuwa chini ya taasisi za serikali kuu.
Akithibitisha hali hiyo,Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Peter Tundu, amesema kuwa asilimia kubwa ya misitu iliyopo katika wilaya hiyo haipo chini ya usimamizi wa halmashauri, bali inasimamiwa na TANAPA kupitia KINAPA na TFS.
“Tuna wajibu wa mazingira kwa mujibu wa sheria, lakini ukweli ni kwamba misitu mingi ipo chini ya KINAPA na TFS,halmashauri ina nafasi ndogo sana ya kufanya maamuzi ya moja kwa moja katika maeneo hayo,” anaeleza Tundu.
Kwa mujibu wake, hali hiyo hufanya usimamizi wa mazingira kuwa mgumu zaidi, hasa pale ambapo jamii zinahitaji kushirikishwa au miradi ya uhifadhi shirikishi inapopaswa kutekelezwa kupitia serikali za mitaa.
TFS yajibu: Teknolojia ipo, lakini uratibu uko wapi?
Akizungumza kwa niaba ya TFS, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dkt. Zainabu Bungwa, amesema licha ya mifumo thabiti ya kisheria, ikolojia ya Mlima Kilimanjaro inakabiliwa na shinikizo kubwa linalotokana na ongezeko la watu na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema takwimu za Global Forest Watch zinaonysha Mkoa wa Kilimanjaro ulipoteza takriban hekta 660 za misitu ya asili mwaka 2024 pekee, hali inayochangiwa na uchomaji moto, ukataji miti kwa ajili ya nishati na upanuzi wa kilimo.
Kwa mujibu wa Dk. Bungwa, TFS inalenga kuongeza uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ikiwemo matumizi ya drones na picha za satelaiti kufuatilia mabadiliko ya uoto wa asili kwa wakati halisi, pamoja na kuimarisha usimamizi shirikishi wa misitu (PFM), miradi ya nishati safi ya kupikia na ushirikiano na mamlaka za serikali za mitaa kulinda vyanzo vya maji.
Hata hivyo, kauli hizi zinaibua maswali
Wakati TFS ikisema usimamizi ni wa pamoja na unahusisha wadau wote, maofisa wa halmashauri wanasema hawana mamlaka ya moja kwa moja katika misitu mingi inayozunguka mlima huo.Ofisa Mazingira wa Moshi Vijijini tayari amethibitisha kuwa halmashauri hubeba wajibu wa mazingira bila kuwa na nguvu ya maamuzi.
Mgongano huu wa kauli unaacha pengo la uwajibikaji,ikiwa ushirikiano upo kama TFS inavyosema, kwa nini mamlaka za mitaa zinasema hazishirikishwi kikamilifu?.Ikiwa jamii ni sehemu ya uhifadhi, kwa nini wananchi wanasema hawapati taarifa wala kushirikishwa katika maamuzi?
Teknolojia inaweza kuonesha kinachopotea, lakini haiwezi kujibu nani anawajibika pale ambapo taasisi hazionekani kufanya kazi kama mfumo mmoja.
Jamii kunufaika kwa kiwango kidogo
Wataalamu wa maendeleo ya jamii wanasema mgawanyo huu wa mamlaka umezipokonya jamii nafasi ya kuwa walinzi wa kwanza wa mazingira yao. Badala ya kushirikishwa kwenye mipango ya pamoja ya uhifadhi, wananchi wanaoishi karibu na misitu hukutana zaidi na marufuku na doria, bila kunufaika moja kwa moja na rasilimali hizo.
Mkazi wa Kirua Vunjo Magharibi, Agnes Enock, anasema licha ya kuishi karibu na msitu wa Mlima Kilimanjaro, hajawahi kushirikishwa katika mikutano wala kupewa taarifa kuhusu nani anayesimamia rasilimali hiyo.
Kwa upande wake, Mwanvita Ally wa Arusha Chini anasema hata alipokuwa mjumbe wa serikali ya kijiji hakuwahi kushuhudia ajenda maalum ya kujadili usimamizi wa msitu uliopo jirani na kijiji chao.
Wananchi hawa wanasema wanachokiona ni doria na marufuku, lakini si ushirikishwaji wala manufaa.
Mapato ya vijiji yashuka
Mmoja wa wenyeviti wa vijiji wastaafu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Moshi amesema zamani vijiji vilikuwa vikikusanya mapato kupitia usimamizi wa misitu, lakini hali hiyo ilibadilika baada ya mamlaka kuhamishiwa taasisi nyingine.
Anasema kijiji chake kilikuwa kikikusanya zaidi ya shilingi milioni 50 kwa mwaka, lakini mapato hayo hayapo tena, hali iliyopunguza motisha ya wananchi kushiriki katika uhifadhi wa misitu hiyo.
Juhudi za kuwapata TANAPA hazijazaa matunda
Katika kuhakikisha uwiano wa taarifa, mwandishi alifanya jitihada za kuwasiliana mara kadhaa na TANAPA ili kupata maelezo yao kuhusu uratibu wa pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi wa misitu ya Mlima Kilimanjaro.
Hata hivyo, hadi makala hii inapochapishwa, juhudi hizo hazikuzaa majibu rasmi.
Kutopatikana kwa kauli ya TANAPA licha ya kufuatiliwa mara kadhaa kunazidisha sintofahamu juu ya namna taasisi hizi zinavyoratibu majukumu yao. Ukimya huu unaongeza uzito wa hoja kwamba licha ya kuwepo kwa taasisi nyingi, bado hakuna uwazi wa pamoja kuhusu nani anawajibika moja kwa moja kwa mustakabali wa misitu ya Mlima Kilimanjaro.
Makala hii inaonesha wazi kuwa changamoto ya ulinzi wa misitu ya Mlima Kilimanjaro haipo kwenye ukosefu wa taasisi, bali kwenye udhaifu wa mfumo wa uratibu na uwajibikaji wa pamoja.
Wakati TFS ikisisitiza usimamizi shirikishi, halmashauri zinasema hazina mamlaka ya maamuzi, na wananchi wanasema hawashirikishwi wala kunufaika. Kauli hizi zinazogongana zinaacha swali moja kuu bila jibu,nani anawajibika kwa rasilimali hii muhimu ya taifa?
Bila mfumo unaounganisha kisheria na kiutendaji TANAPA, TFS na serikali za mitaa, misitu ya Mlima Kilimanjaro itaendelea kupotea katika kivuli cha taasisi nyingi, lakini bila uwajibikaji mmoja unaoonekana wazi.
Katika mazingira haya, swali si kama taasisi zipo bali kama zinafanya kazi kwa pamoja. Na kadri majibu yanavyoendelea kutofautiana, ndivyo misitu ya Mlima Kilimanjaro inavyoendelea kupotea kimya kimya, chini ya usimamizi wa taasisi nyingi lakini bila uwajibikaji mmoja ulio wazi

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama