Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Nzega
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Nzega (NZUWASA) imeongeza mtandao wa upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Mji wa Nzega hadi kufikia kilomita 738.3 ambazo ni sawa na asilimia 99.5 ya eneo lote.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Humphrey Mwiyombela amesema kuwa takribani eneo lote la Mji wa wa Nzega kwa sasa limefikiwa na huduma ya maji safi na salama.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na mikakati yao ya kuendelea kuzalisha maji kupitia vyanzo vyake vya ndani kwa lengo la kupanua wigo wa upatikanaji huduma hiyo katika maeneo yote ya mji huo na maeneo jirani.
Ametaja mkakati mwingine uliosaidia kuimarisha upatikanaji huduma hiyo kuwa ni kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (KASHWASA).

Amesema,mahitaji ya maji kwa wakazi wa mji huo kwa siku ni lita za ujazo 5,600 na kiasi kinachozalishwa kupitia vyanzo vya ndani ni lita za ujazo 2,100 kwa siku na kiasi kinachonunuliwa KASHWASA ni lita 3,500.
“Hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Mji wa Nzega na maeneo jirani imeimarika zaidi, wakazi wa Nzega sasa wanapata maji safi na salama ya kutosha kila siku, hakuna changamoto yoyote,” ameeleza.
Ili kuhakikisha mji huo unakuwa na mfumo mzuri wa uondoshaji maji taka katika makazi ya watu,mamlaka imetekeleza mradi wa mabwawa ya kupokea na kutibu maji taka yenye lita za ujazo 1,200, mradi huu umegharimu shilingi bilioni 1.5.
Mhandisi Mwiyombela amefafanua kuwa mradi huo ni muhimu kwa kuwa utaongeza ufanisi wa usafi na kuboresha mazingira ya mji huo, ambapo Januari pekee wamemwaga tripu 84 za majitaka, zenye lita za ujazo 783.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi