Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Kagera
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imewahaidi wawekezaji wazawa kuwa itaanzisha madawati ya uwekezaji kila Halmshauri za WIlaya, ili kurahisisha hatua za kuanza uwekezaji.
Ambapo itaunganisha kwa pamoja taasisi zinazohusiana na usajili wa masuala ya uwekezaji ili kutoa huduma kupitia dawati hilo.

Hata hivyo TISEZA inaendelea na kampeni maalum ya kuhamasisha uwekezaji kwa lengo la kusogeza huduma za uwekezaji hadi ngazi ya mikoa na halmshauri ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Akizungumza katika kongamano la wadau wa uwekezaji wa ndani mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Balozi Azizi Mlima, amesema taasisi hiyo imelenga kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi ili kuwawezesha kupata unafuu wa mitaji.
Pia kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu za uwekezaji ikiwemo kuwapunguzia adha wawekezaji kwa kuweka dawati moja la kupata huduma zote.
Ameeleza kuwa licha ya changamoto ya uelewa mdogo wa uwekezaji kwa baadhi ya Watanzania, elimu na mipango ya TISEZA imeanza kuzaa matunda kwa kuwahamasisha wananchi kuwekeza zaidi ndani ya nchi, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kukuza uzalishaji wa ndani.
Amesema TISEZA inaangazia fursa mbalimbali Kanda ya Ziwa ikiwemo Mkoa wa Kagera ambapo kuna fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo,Kilimo cha mazao ya biashara kama maparachichi,ufugaji wa kisasa,ufugaji wa samaki.
Uongezaji thamani wa mazao ya kilimo ambapo wananchi wamekumbushwa umuhimu wa kumiliki hati za nyumba na viwanja, kama nyenzo muhimu ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha na kuanzisha au kupanua miradi ya uwekezaji.
Nao baadhi ya wawekezaji ambao wameshiriki kongamano hilo wamepongeza hatua muhimu za TISEZA kuona umuhimu wa kufikisha elimu na kuweka mpango wa kufungua madawati ya uwekezaji kwa ngazi ya halmashauri kama hatua muhimu ya kutambua changamoto zao katika uwekezaji na kurahisisha hatua za kujisajili.



More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama