March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Itunda aonya wazazi wanaokaidi agizo michango ya chakula shuleni

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewaagiza watendaji wa kata na maafisa tarafa kuhakikisha kila mzazi anatimiza wajibu wa kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni kama ilivyoelekezwa, huku akionya kuwa wazazi watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Itunda ametoa kauli hiyo Februari 7, 2026, wakati wa kikao maalum cha wadau wa elimu cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya kilicholenga kujadili masuala muhimu ya kuboresha sekta ya elimu na ustawi wa wanafunzi.

“Kikao hiki kina lengo kubwa la kujadili kwa kina hali ya utoaji wa chakula shuleni ili kuleta tija katika ujifunzaji na kuongeza matokeo chanya ya kitaaluma kwa watoto,” amesema Itunda.

Amesisitiza kuwa wazazi na walezi wana wajibu wa kuchangia chakula ili kuhakikisha watoto wanakuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kuongeza umakini darasani.

Kikao hicho pia kilijadili mikakati ya kuinua kiwango cha ufaulu katika shule za Jiji la Mbeya, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa taaluma, kuongeza ushirikiano kati ya walimu, wazazi na viongozi wa maeneo husika, pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya wanafunzi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewapongeza walimu wa Jiji la Mbeya kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kufundisha na kulea wanafunzi, akitambua mchango wao muhimu katika kujenga rasilimali watu na kuendeleza taifa.

Aidha, Itunda amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na kuimarisha maslahi ya walimu—hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji nchini.