Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Tabora
ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM),kwa miaka 15, Munde Tambwe amezikwa jana katika makaburi ya Shehe Yahaya, Kata ya Ng’ambo Mjini Tabora na kuhitimisha safari yake hapa duniani.
Msiba huo umevuta hisia za watu wengi wakiwemo vijana, akinamama, wana CCM, jamii, wabunge na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, kutokana na ushirikiano wake,ukarimu na kujitoa zaidi kwa jamii enzi za uhai wake.

Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye msiba huo, Makamu wa Rais Dkt.Emanuel Nchimbi ameeleza kuwa marehemu alikuwa rafiki wa kila mtu.
Ameongeza kuwa alikuwa mtu mwema kwa jamii, wanaCCM, wabunge na viongozi wenzake na katika nafasi zote alizowahi kutumikia alitanguliza maslahi ya nchi na chama chake na hakuwa na makuu.
“Rais Samia metoa pole kwa wanafamilia, jamii, wabunge na wanaCCM wote kwa kuondokewa na mtu muhimu na kada mwaminifu kwa chama chetu,”amesema.
Ameongeza kuwa licha ya kupumzika ubunge baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana, marehemu aliendelea kutumikia jamii kwa kujenga nyumba ya kuabudia waislamu ingawa bado hajakamilisha.
“Rais ameahidi kutoa shilingi milioni 30 na mimi nitatoa shilingi milioni 10 ili kuchangia ujenzi wa msikiti aliokuwa anaujenga marehemu Munde na nyumba iliyopo katika eneo hilo na wengine tuendelee kuchangia,”.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Mbunge wa Viti Maalumu Mary Chatanda akitoa salamu kwenye mazishi hayo, amesema kuwa marehemu Munde alijitoa kusaidia wanawake na vijana.
Alihamasisha wanawake na vijana wengi zaidi kujitokeza kugombea nafasi za ubunge wa majimbo na viti maalumu na katika uchaguzi mkuu uliopita wanawake na vijana wengi zaidi walijitokeza kuwania ubunge na udiwani.
Wakiongea kwa niaba ya Wabunge wenzao, Nape Nnauye (Mbunge wa Mtama, Lindi) na Hussein Bashe wa Nzega (Tabora) wamesema kuwa marehemu alikuwa mzalendo wa kweli kwa chama na serikali.

“Katika nafasi zote alizowahi kutumikia ikiwemo Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Kamati Kuu, hakuwa na chembe yoyote ya usaliti kwa chama chake,”amesema Nape.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa,Saidi Nkumba amekiri kuwa CCM imetikiswa kwa kundokewa na watu wawili muhimu sana ndani ya wiki moja, Mzee Nassoro Hamdani Meddy (mmiliki wa mabasi ya NBS) na dada Munde Tambwe.
Ameeleza kuwa viongozi hao walikipenda sana Chama Cha Mapinduzi na walijitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha kinafanikisha mipango yake yote ikiwemo kushinda chaguzi zilizokuwa mbele yao.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina