Na Jackline Mkota,Timesmajira
MKURUGENZI wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Ferdinand Kabyemela, ametangaza kurejea rasmi sokoni kwa application ya Swifpack baada ya kufanyiwa maboresho makubwa ya kiufundi na kiuendeshaji, akisema sasa imekuwa imara zaidi, ya kisasa na yenye manufaa mapana kwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam, Kabyemela amesema toleo jipya la Swifpack limeboreshwa ili kukidhi mahitaji halisi ya soko la Tanzania, huku likiongeza ufanisi wa mfumo, kuimarisha mawasiliano kati ya abiria na madereva, kurahisisha na kulinda malipo pamoja na kuboresha huduma kwa wateja na usalama wa watumiaji.
Amefafanua kuwa kupitia Swifpack, wateja sasa wanaweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo usafiri wa abiria, usafirishaji wa vifurushi, mizigo midogo na mikubwa pamoja na huduma za courier kwa biashara na taasisi.
Aidha, amesema jukwaa hilo linatoa chaguo pana la vyombo vya usafiri kuanzia pikipiki, bajaji, magari madogo na ya mizigo hadi magari makubwa yenye uwezo wa kubeba mizigo ya hadi tani 30.
Kabyemela amesisitiza kuwa Swifpack si application ya usafiri pekee bali ni suluhisho la kitaifa la ajira kwa vijana, linalolenga kuwawezesha madereva, wamiliki wa vyombo vya usafiri na wajasiriamali kupata kipato na soko rasmi, sambamba na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Kwa upande wa madereva, amesema toleo jipya la Swifpack limezingatia ustawi wao kwa kutoa makato madogo ya matumizi ya mfumo, upatikanaji wa bima ya afya, fursa za kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na mfumo wa subscription unaowawezesha kupata simu janja kwa utaratibu nafuu, huku malipo yakifanyika kwa uwazi na uhakika.
Akizungumzia manufaa kwa abiria na wateja, Kabyemela amesema wanufaika wa Swifpack watanufaika na bei shindani, usalama na ufuatiliaji wa safari, huduma ya haraka na ya kuaminika pamoja na ofa mbalimbali zinazotolewa mara kwa mara.

Katika wito wake kwa umma, amewahimiza abiria kupakua na kutumia upya application ya Swifpack, madereva kujisajili kwa wingi, wafanyabiashara kuitumia kwa usafirishaji wa bidhaa zao na taasisi kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania kupitia huduma hiyo rasmi ya kitaifa.
Amemalizia kwa kusisitiza kuwa kurejea kwa Swifpack ni kwa nguvu mpya, akisema Shirika la Posta Tanzania litaendelea kutoa huduma bora, za kisasa na zenye tija kwa maendeleo ya taifa.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi