March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kuimarisha jeshi la uhifadhi,kuboresha maslahi ya askari

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Hassan Abbasi,amesema Serikali itaendelea kuimarisha Jeshi la Uhifadhi pamoja na kuboresha maslahi ya askari wa uhifadhi nchini kwani ni kundi muhimu ambalo linalida rasilimali za nchi.

Dkt.Abbasi,amezungumza hayo Februari 2,2026,wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya kijeshi kwa askari wapya 256 wa TAWA, yaliofanyika katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi mkoani Mwanza.

Ambapo amesema jeshi la Uhifadhi kwa sasa lina askari zaidi ya 8,800 waliopo maeneo mbalimbali nchini huku kwa mwaka 2025 Serikali imefanikiwa kuajiri zaidi ya askari wa uhifadhi 990 kati hao TAWA 403,TANAPA 229, TFS 369.

Amesema vijana wote walioajiriwa tayari wapo kazini, huku Serikali imetoa upya vibali vya ajira kwa taasisi za uhifadhi.

“Serikali itaendelea kutimiza yale ambayo inapaswa kufanya,mkakati mingi tunatoa ya kuendelea kuimarisha taasisi zetu na kuendelea kuajiri watumishi.Tangu mwaka huu wa 2026 ulivyoanza Serikali imetoa tena vibali vipya vya ajira ambapo TAWA wamepewa tena kibali cha kuajiri askari wa uhifadhi 294, TANAPA 115, TFS 300,kwaio jumla kwa kipindi hiki ni zaidi ya ajira 709 zimetolewa,”amesema Dkt.Abbasi.

Hivyo amewataka vijana wa kitanzania kuacha woga pindi zinapotikea nafasi kama hizo pamoja na kutokubali kudanganyana mtandaoni kuwa nafasi hizo zinapotangazwa zinakuwa na watu tayari na badala yake kama wanasifa wajaribu bahati kwani Serikali imeweka mfumo mzuri.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),Mlage Kabange,amesema kwa kipindi hicho wamepokea ajira mpya ya askari wa uhifadhi 550 kati yao ni hao waliohitimu mafunzo hayo ambao ni 256 huku wengine 294 wanatarajia kuanza mafunzo.

Ambapo amesema,idadi hiyo ya askari wapya inaongeza utendaji kazi kwa TAWA,nguvu ya kuhifadhi na kulinda maeneo yote ya rasilimali za nch huku akisisitiza kuwa mamlaka hiyo hiyo inakaboliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ujangiri na uvamizi wa maeneo ya uhifadhi kutokana na shughuli za kibinadamu.

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo,Mkufunzi Mkuu,Ofisa Uhifadhi daraja la pili TAWA,Amani Nasoro,amesema mafunzo hayo ya kijeshi yametolewa kwa askari wapya ya TAWA 256 kati yao wanaume ni 222 huku wanawake wakiwa 34, ambayo yamedumu kwa kipindi cha miezi sita tangu Julai 22,2025 hadi Februari 2,2026.

Amsema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea askari uwezo wa udhibiti wa wanyamapori, matumizi sahihi ya ramani na GPS, pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za porini.

Mkuu wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Mwanza,Jeremiah Msigwa,,amewahimiza askari hao kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia uzalendo pamoja na taratibu,kanuni na sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Amiri Mkalipa,amesema,wahitimu hao no jicho,sikio,mkono na mguu wa Serikali hivyo amewahimiza wakafanye kazi kwa uzalendo,sheria na taratibu pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA,Hamis Semfuko, amesema “Nendeni mkafanye kazi kwa uzalendo na nidhamu ili kufikia malengo,hatua mliofikia ni muhimu sana katika kutengeneza historia ya maisha yenu,ninyi ni askari,ni walinzi mnaotegemewa na taifa hili.Kuanzia leo hadi ukomo wa utumishi wenu utakuwaje,hii inatitajika nidhamu,uzalendo na uwajibikaji ili kufanikiwa,”.