March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nywila(Password) Bora ni Ipi? ‘rgeihggkjgkggjgfdkffkfkf’ au ‘Axr!.12*=?’

Mwandishi: Ismail Mayumba


Nywila ni neno la siri linalotumiwa kumtambua mtumiaji halali wa mfumo na kulinda akaunti au taarifa binafsi zisifikiwe na mtu asiyehusika. Ni neno ambalo mtumiaji hulibuni kwa upekee wake, ili mtu mwingine asiweze kulifahamu kirahisi. Nywila hubaki kuwa siri kati ya mtumiaji na mfumo anaoutumia. Hata mtengenezaji wa mfumo hawezi kuijua nywila ya mtumiaji, kwa sababu inapohifadhiwa hubadilishwa kuwa mfumo wa usimbaji (encryption), ambapo huonekana kama mchanganyiko wa namba na alama zisizoeleweka.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la matukio ya watu kudukuliwa akaunti zao kutokana na nywila zao kutambulika kwa urahisi. Hali hii imewafanya wataalamu wa usalama wa mifumo kushauri watumiaji kuweka nywila ngumu na salama zaidi. Kutokana na hilo, swali muhimu hujitokeza: ni ipi hasa nywila yenye nguvu?

Watumiaji wengi huamini kuwa nywila ndefu ndiyo nywila yenye nguvu zaidi, kwa sababu mwizi au mdukuzi atachukua muda mrefu kuijua. Ingawa urefu wa nywila una mchango fulani katika usalama, si kigezo cha kutosha peke yake. Mara nyingi, nywila ndefu humfanya hata mwenyewe kuisahau, hasa pale anapolazimika kutotumia mfumo mara kwa mara. Hali hii humlazimu kuiandika mahali, jambo ambalo huongeza hatari ya kuvuja kwa usalama.

Zaidi ya hapo, nywila ndefu ambayo inahusisha majina ya kampuni, ndugu, marafiki au vitu anavyovipenda mtumiaji huwa rahisi kutabirika. Hata kama nywila hiyo imetengenezwa kwa herufi nyingi zisizo na maana, au kwa namba tupu pekee, bado huwa rahisi kwa mifumo ya kiteknolojia kuivunja. Kwa mantiki hiyo, aina hii ya nywila huwa dhaifu, sawa na povu la sabuni—unapoligusa tu, linayeyuka.

Nywila yenye nguvu kwa kweli ni ile yenye mchanganyiko wa vipengele tofauti. Inapaswa kuwa na herufi kubwa na ndogo, namba, pamoja na alama maalum kama alama ya mshangao au nyota (*). Aidha, nywila bora isiwe fupi kupita kiasi wala ndefu kupindukia; urefu wa herufi sita hadi kumi na mbili huchukuliwa kuwa mzuri zaidi. Mchanganyiko huu humfanya mtumiaji aweze kuikumbuka kwa urahisi, huku ikibaki kuwa ngumu sana kwa wadukuzi kuipasua.

Kwa kuzingatia vigezo hivi, kati ya nywila mbili zilizotajwa, ‘Axr!.12=’* ndiyo nywila yenye nguvu zaidi kuliko ‘rgeihggkjgkggjgfdkffkfkfkfkfjjjffffd’. Ingawa ya kwanza ni fupi, ina mchanganyiko sahihi wa herufi, namba na alama maalum, jambo linaloifanya kuwa salama zaidi.

Kwa ujumla, kuwa na nywila ndefu bila kufuata vigezo vya usalama ni kama kuwa na kinga dhaifu. Ubora wa nywila haupimwi kwa urefu wake pekee, bali kwa mchanganyiko wake. Nywila iliyoandaliwa vizuri humlinda mtumiaji dhidi ya hatari nyingi za kiusalama katika ulimwengu wa kidijitali.