September 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lukuvi awashukia wanasiasa wanaotuhumu viongozi kupora ardhi

Na Munir Shemweta, TimesMajira Online, Iringa

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amekanusha vikali kauli iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuwa, kuna baadhi ya viongozi wamepora ardhi ikiwemo ardhi ya eneo la Mbarari mkoa wa Mbeya na kusisitiza kuwa kati ya viongozi waliotuhumiwa hakuna hata kiongozi mmoja aliyepora ardhi.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi amesema umilikishaji ardhi nchini unafuata sheria na serikali haina ubaguzi katika kumilikisha mtu yeyoye ardhi huku akiweka wazi kuwa umilikishaji kwa mtu yeyote hauna kikomo.

Lukuvi amekanusha uvumi huo leo alipokutana na waandishi wa habari mkoani Iringa akitolea ufafanuzi wa baadhi ya kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa vyama vya siasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

“Serikali ya awamu ya tano haina ubaguzi wa kumilikisha ardhi na mwananchi yeyote bila kujali itikadi ya chama cha siasa anaweza kumilikishwa,” amesema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, Seriali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kushughulikia masuala ya ardhi ikiwemo lile la kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa kwenye hifadhi na kubainisha kuwa, serikali inaangalia namna ya kuvibakisha vijiji vingine 55 vilivyosalia.

Akitolea ufafanuzi suala la Mbarari, Lukuvi amesema wananchi wanaoishi katika vijiji 29 eneo la Mbarari wameamuriwa kubaki eneo hilo ingawa kwa mujibu wa GN Namba 28 ya mwaka 2008 walitakiwa kuondoka lakini kwa huruma ya Rais John Pombe Magufuli alibatilisha uamuzi huo na kuagiza vijiji visiondolewe.

“Wananchi wa Mbarari waendelee kuishi kama wanavyoendelea, Mgogoro wa Mbarari ni wa muda mrefu tangu mwaka 2008 na serikali ya awamu ya tano haipaswi kulaumiwa na Rais Magufuli siyo mtu wa kubeza kwa kuwa vijiji vilitakiwa kuondolewa lakini aliamuru vibaki” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema, baada ya uamuzi wa kutoviondoa vijiji 920 kati ya 975 hatua inayofuata ni kupima upya mipaka sambamba na kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kubainisha matumizi ya maeneo ya maeneo husika.

Vile vile, Lukuvi amesema serikali katika kuwajali wananchi imeamua pia kufuta mapori tengefu 12 yenye zaidi ya hekta 707,659.4 sambamba na kumega hifadhi 14 za misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

Lukuvi ameongeza kwa kusema, serikali ya awamu ya tano imeendelea kuchukua hatua za kupunguza na kufuta mashamba makubwa kwa wamiliki waliokiuka masharti ya umiliki na kubainisha kuwa, kwa sasa serikali imeshafuta mashamba yasiyopungua 49 na kugawiwa kwa wananchi.

Akigeukia tatizo la ardhi katika mkoa wa Morogoro, Waziri Lukuvi amesema kazi ya uhakiki mashamba 11 katika eneo la Kilosa imekamilika na muda ukiruhusu watatangaziwa mashamba yaliyofutwa kutokana na wamiliki wake kukiuka masharti ya umiliki.

Hata hivyo Lukuvi ametoa onyo kwa wananchi wote waliomilikishwa ardhi kuhakikisha wanafuata sheria na kusisitiza kuwa, sheria za ardhi zimewekwa ili kutekelezwa na wasiozifuta watafutiwa umiliki na kupatiwa watu wengine.