Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa msaada wa vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Nsalala, iliyopo Wilaya ya Mbeya, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa, Januari 27.
Msaada huo unahusisha karatasi za nukta nundu (Braille), vifaa vya kurekodia kwa ajili ya wanafunzi wenye changamoto ya usikivu hafifu, pamoja na kompyuta mpakato.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa Januari 26, 2026 kwa Mkuu wa Shule ya Msingi Nsalala na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mtendaji Erica Yegella alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum katika siku yake ya kuzaliwa.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum. Katika siku yake ya kuzaliwa ameona umuhimu wa kuwapatia vifaa hivi muhimu, hivyo leo tumejumuika pamoja na wanafunzi kupokea msaada huu,” amesema Yegella.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Nsalala, John Malila, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,194, ambapo kati yao 49 ni wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Malila amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa mchango huo, akisema kuwa hatua hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa watoto wenye mahitaji maalum ambao hapo awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa za kushiriki masomo.
“Hapo awali baadhi ya watoto walikuwa wakifungiwa ndani, lakini sasa kupitia juhudi za Rais Samia, watoto hawa wamepata fursa ya kushiriki kikamilifu katika masomo,” amesema Malila.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia pia amewezesha ujenzi wa bweni shuleni hapo, litakalosaidia wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali na mazingira magumu kuishi karibu na shule.
“Bweni hili litasaidia wanafunzi kukaa shuleni na kufuatilia masomo kwa urahisi. Vifaa vilivyotolewa vitamsaidia pia mwalimu wa elimu maalum, Shija, kuhakikisha watoto hawa hawaachwi nyuma kielimu,” amesema.
Akizungumzia hali ya taaluma, Malila amesema shule ya Nsalala inaendelea kufanya vizuri na imeweka mikakati ya kuimarisha zaidi ufaulu wa wanafunzi.

Kwa upande wake, Baraka Kajiba, mwanafunzi asiyeona katika Shule ya Msingi Nsalala, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa msaada huo na kumuahidi kufanya vizuri zaidi katika masomo.
Naye Ofisa Elimu Awali na Msingi wa Wilaya ya Mbeya, Tanu Kameka, amesema msaada huo umeonesha namna Rais Dkt. Samia anavyothamini watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwaletea vifaa saidizi vya kisasa.
“Shule ya Nsalala ni shule jumuishi. Tuna shule nyingine zenye vitengo vya elimu jumuishi kama Mbalizi One, Juhudi na Nsongwi Juu. Vifaa hivi vitakuwa msaada mkubwa kwa watoto na walimu,” amesema Kameka.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi