Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
Waziri Mkuu,Dkt.Mwigulu Nchemba, amewaagiza Mawaziri wa Wizara zote kufanya tathmini ya kina ya miradi yote inayotekelezwa na Serikali nchini, ili kubaini wakandarasi ambao hawajalipwa malipo ya awali (advance payment), hali inayosababisha kusimama kwa utekelezaji wa miradi.
Dkt. Nchemba alitoa agizo hilo Januari 23,2026,jjijini Mwanza, mara baada ya kuzindua meli ya MV New Mwanza,ambapo amesema kuwa katika maeneo mengi aliopita, amebaini miradi iliyokwama kwa sababu wakandarasi wamesaini mikataba na kupewa kazi lakini hawajalipwa fedha za awali.
“Katika kupitapita maeneo mengi, mkandarasi ametoka site, amesaini mkataba, amepewa kazi lakini hajalipwa. Lazima tufanye jambo katika eneo hili,hivyo nawaagiza fanyeni tathmini ya miradi yote,”amesema Dkt.Nchemba.
Amesema baada ya tathmini hiyo kukamilika, Wizara ya Fedha ipitie upya mafungu yote ya matumizi, hususani tunapoelekea nusu mwaka wa fedha, isipokuwa yale ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na sekta ya afya, ili kubaini matumizi yasiyo na athari kwa wananchi na kuyakata na fedha zake zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo.
“Yale matumizi ambayo hayatuathiri, yakatwe yaelekezwe kwenye miradi ya maendeleo. Zipo fedha ambazo hazituathiri, najua mianya yake, mnatengeneza kalenda na kutumiana, tumieni hata za kwenye simu,” amesema.
Amesema serikali inaendelea kupata hasara kubwa kutokana na matumizi ya mazoea yasiyo na tija, huku Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameishatoa maelekezo ya kuachana na matumizi ya karatasi na kuhamia kwenye teknolojia ya kidijitali ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.
“Lazima tupate fedha,hata kama taasisi na mashirika ya umma tayari mmekwishatoa gawio, kateni fedha tuzipeleke kwenye mambo ya msingi,nitaitisha kikao maalum cha Wizara ya Fedha na kuhudhuria mwenyewe,”.
Aidha, Dkt. Nchemba amesema agizo hilo linahusu pia ngazi za mikoa, miji na halmashauri, akisisitiza kuwa maeneo mengi yana fursa za wananchi kuchangia maendeleo kupitia shughuli zao za kiuchumi, hususani ujenzi wa masoko kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.
Hivyo amezitaka halmashauri kutenga maeneo rafiki kwa shughuli za wananchi badala ya kuwapeleka katika maeneo yasiyofaa, akikumbusha kuwa Rais Samia aliongeza asilimia nne ya mapato ya ndani ili halmashauri ziweze kuboresha huduma na miundombinu ya wananchi.
“Wakuu wa mikoa na halmashauri ziwe busy na mambo yanayowahusu wananchi. Ndiyo maana tuligatua madaraka. Mameya na wenyeviti wa halmashauri msifanye kazi ya kugawana madaraka miaka yote mitano,” alisema.
Akigusia migogoro ya ardhi na changamoto za wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, Waziri Mkuu alisema ni lazima Serikali ipange matumizi bora ya ardhi ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kukimbilia kwa viongozi mara kwa mara.
“Tunataka viongozi na watumishi wa kuchaguliwa wawe busy na mambo yanayowagusa wananchi. Kwingine wananchi wanahangaika hadi waende kwa viongozi, hilo halikubaliki,” alisisitiza.
Sanjari na hayo amewataka wakuu wa mikoa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo hayo katika taasisi zote za umma, mashirika ya umma na serikali za mitaa, ili kuondoa matumizi ya mazoea na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye tija, kuongeza mapato na kuboresha ustawi wa wananchi.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi