*Aweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa vituo vya kusukuma maji, matenki na mabomba makuu.
*Asisitiza uwajibikaji kwa watendaji huku mradi ukitarajiwa kunufaisha wananchi 450,000 wa Mwanza
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt.Mwigulu Nchemba,amewaahidi wananchi wa Nyamagana na Mkoa wa Mwanza kuwa atahakikisha mradi wa ujenzi wa vituo vya kusukuma maji,mabomba makuu ya usafirishaji maji na matenki ya kuhifadhia maji unakamilika kwa wakati.
Huku akiwasisitiza watendaji uwajibikaji na mshikamano kwa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Dkt.Nchemba, amezungumza hayo Januari 23,2026, wakati akiweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa vituo vya kusukuma maji,mabomba makuu ya usafirishaji maji na matenki ya kuhifadhia maji wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Ambapo amesema,ili maji yafike kwa wananchi kuna hatua lazima zitekelezwe,hatua ya kwanza ni kujenga chanzo cha maji ambapo Serikali imeisha fanya kwa kujenga chanzo cha maji Butimba.
Hatua ya pili ni ujenzi wa matenki huku hatua ya tatu ambayo itafuata ni usambazaji wa maji ili wananchi waweze kuyapata nyumbani.
“Nitasimamia kwa ukaribu na kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili yawafikie wananchi.Tueendelee kulinda amani ya nchi yetu,haya yote mazuri tunayoyasema hatuwezi kutekeleza kama hatuna amani,”amesema Dkt.Nchemba.
Kwa upande wake Waziri wa Maji,Jumaa Aweso,amesema yeye na timu ya Wizara hiyo hawatokuwa kikwazo cha Wananyamagana na Mwanza kutopata maji.
Amesema mradi huo unaotarajiwa kukamilika Desemba,2026 huku akisisitiza kuwa utakamilika kwa wakati.”Mkandarasi ana kisingizio cha kutokamilisha mradi huu kwa wakati kwani fedha zipo,jukumu lake ni kuongeza nguvu kazi,”amesema Aweso.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),Neli Msuya,amesema mradi huo ulianza kutekeleza Desemba 2024 na unatarajia kukamilika Desemba,2026 utakaonufaisha wananchi takribani 450,000 wa Jiji la Mwanza na Wilaya za Magu na Misungwi, ikiwemo Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyahingi, Luchelele, Sahwa, Kishiri, Igoma, Kisesa, Bujora, Kanyama, Fela na Usagara.
“Mradi umegharimu kiasi cha bilioni 46.2 ambao unahusisha ujenzi vituo viwili vya kusukuma maji,matenki matano ya kuhifadhia maji pamoja na mabomba makuu ya usambazaji maji,”amesema Neli.
Naye Diwani wa Kata ya Lwanhima,Chanila Mwakyoma,amesema,katika Kata hiyo wanachamgamoto ya maji katika mitaa 18 na wananchi wananunua dumu la lita 20 kwa shilingi 500.
“Fikiria familia moja yenye watu watano au sita,itakidhi maji ya kiasi gani na inapunguza kipato cha ndani ya familia,tunaamini mradi huu utatatua changamoto kwa wananchi juu ya maji.Tunaomba Serikali uweze kusukuma mradi huu ili ukamilike,”amesema Chanila.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Isamilo, Charles Nyamasiriri,kupitia miradi hiyo inakwenda kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Mwanza ambalo kwa sehemu kubwa mazingira yake ni milima.
“Matenki haya yakikamilika yanaenda kutatua changamoto ya maji.Wananchi kipindi hiki mradi unapo endelea waendelee kutunza maji pale yanapo toka,naamini mradi utakamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa,wito wangu kwa mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuongeza kasi kwani tunahitaji maji ambayo ni uhai,”amesema Nyamasiriri.

Mkazi wa Sahwa Nyakerongo Nyitika,amesema mradi huo ulikamilika utawasaidia kwani kwa sasa wanahangaika kutafuta maji kwenye visima na wakati mwingine yanakauka.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi