Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetoa kipindi cha nyongeza cha miezi mitatu kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi ambazo bado hazijakamilisha usajili, kukamilisha zoezi hilo kwa hiari.
Hatua hiyo inatokana na maagizo yaliyotolewa Januari 8, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, yakilenga kuimarisha ulinzi wa haki ya faragha ya wananchi katika matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam Januari 22,2026,Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema kipindi hicho cha nyongeza kimeaanza Januari 8 hadi Aprili 8, 2026.
Amesema taasisi zote nchini zinapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha zinasajiliwa, zinaimarisha mifumo yao ya ulinzi wa taarifa binafsi na kuzingatia kikamilifu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.
“Muda huu wa nyongeza haumaanishi kusitishwa kwa utekelezaji wa sheria, bali ni fursa ya mwisho ya hiari kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya taasisi zitakazobainika kukiuka matakwa ya sheria hiyo,” amesema. Dkt. Mkilia.
Ameongeza kuwa baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, PDPC itaanza kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria kwa taasisi za umma na binafsi zinazokusanya, kuhifadhi, kuchakata au kusafirisha taarifa binafsi ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mkilia, ukaguzi huo utalenga kubaini ukiukwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kanuni zake, ikiwemo matumizi ya taarifa binafsi bila ridhaa ya wahusika au uvunjaji wa faragha ya wananchi.
Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu, taasisi au kampuni itakayobainika kukiuka sheria hiyo, ikiwemo kutozwa faini, kifungo au adhabu zote kwa pamoja na kulipa fidia kwa waathirika wa ukiukwaji huo.
Dkt. Mkilia amesisitiza kuwa uwajibikaji huo utazingatia usawa bila kujali hadhi au ukubwa wa taasisi au mtu anayekiuka sheria.
Katika hatua nyingine, amesema PDPC itaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa mwaka 2026, itakayofanyika kuanzia Januari 26 hadi 30, huku kilele chake kikiwa Januari 28.
Amesema katika kipindi hicho, Tume itatekeleza programu mbalimbali za elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, mafunzo kwa taasisi za umma na binafsi pamoja na ziara za kutoa elimu kwa wananchi.
“Maadhimisho haya yanalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za faragha, kuhimiza uwajibikaji wa taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi, na kujenga utamaduni wa kulinda faragha katika matumizi salama ya teknolojia na huduma za kidijitali,” amesema
Dkt. Mkilia ameongeza kuwa PDPC itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, weledi na bila upendeleo kwa lengo la kulinda taarifa binafsi za Watanzania.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi