Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),mkoani Tabora wanatarajia kutengeneza barabara zenye urefu wa Kilomita 114.05 kwa gharama ya sh bilioni 7.4 katika Wilaya ya Tabora Mjini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Hayo yamebainishwa j na Meneja wa TARURA Wilaya ya Tabora, Mhandisi Subira Manyama, alipokuwa akiwasilisha rasimu ya mapendekezo ya bajeti ya TARURA kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mhandisi Manyama amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wanatarajia kutumia kiasi hicho cha fedha Kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa km 114.05 na kujenga makalavati 11, boksi kalavati 10 na vivuko 11.
Watajenga mifereji yenye urefu wa mita 3,300 kwa fedha za mfuko wa barabara, barabara ya kiwango cha zege km 0.1, changarawe km 3.98, makalavati mistari 19, vivuko 24 na mifereji mita 4,250 kwa fedha za tozo ya mafuta.
Pia watatengeneza km 11.5 za changarawe, boksi kalavati 1 na makalavati 5 kwa fedha za Mfuko wa Jimbo na matengenezo ya km 3.2 za barabara ya lami na mita 1200 za mifereji kwa fedha za Mfuko wa Barabara.
Akifafanua mpango wa matengenezo ya barabara hizo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund) amesema kuwa watafanya matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa km 98.8 kwa gharama ya sh milioni 348.9.
Aidha milioni 230.5 zitatengeneza barabara korofi km 7.04 na sh milioni 162.6 matengenezo ya muda maalumu km 8.13 huku sh milioni 475 zikitumika kujenga makalavati, mifereji, vivuko na barabara za mlisho na mkusanyiko.
Sanjari na hayo amesema vipaumbele vya rasimu hiyo kuwa ni kukarabati barabara zote ambazo zimekuwa hazipitiki kwa kipindi kirefu ili ziweze kupitika wakati wote, kuzifanyia matengenezo barabara zote za mjini na vijijini ili ziwe imara zaidi.
Amesema,watafanya matengenezo ya kawaida kwa sehemu korofi zote na ya muda maalumu kwa baadhi ya barabara ili kuwezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mazao yao kutoka vijijini kwenda kwenye masoko kwa mwaka mzima.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi