March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA Dodoma yawahakikishia ukarabati barabara korofi Chinyoyo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma 

HALI ya Miundombinu  ya Barabara nyingi katika Mtaa wa Chinyoyo kata ya kilimani Jijini Dodoma zimekuwa hazipitiki katika kipindi cha masika jambo ambalo hupelekea wananchi wa mtaa huo kushindwa kupita katika barabara hizo katika kipindi cha masika.

Kutokana na changamoto hiyo Meneja wa Wakala  wa Barabara  za Vijijini  na Mijini (TARURA) wa Wilaya ya Dodoma Mhandisi  Emmanuel Mfinanga kulichukulia kwa uzito jambo hilo ambapo aliahaidi ndani ya muda mchache ataagiza wataalamu wake kwenda kukagua Miundombinu ya barabara hizo.

Mha.Mfinanga ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Diwani wa kata ya kilimani ofisini kwake Januari 21,2026.

“Hizo barabara za Mtaa wa Chinyoyo ninazifahamu vizuri sana na changamoto zake zote ninazifahamu kubwa miundombinu ya barabara za Mtaa wa Chinyoyo ni ndogo barabara nyingi ziko chini ya mita nne hivyo hata uingizwaji wa mitambo yetu inakuwa ni changamoto kubwa kwani mitambo yetu walau ili iweze kuingia vizuri walau barabara hizo zingekuwa zina mita kuanzia mita sita, lakini nikuhakikishie Mhe Diwani nitapita na wataalamu wangu ndani ya siku mbili hizi ili tuweze kuziona na kushauriana kwa pamoja jinsi ya kuziboresha walau wananchi waweze kunitumia barabara hizo” amesema Mfinanga

Aidha Meneja huyo amesema kata zote 41 za wilaya ya Dodoma Mjini kumekuwa na changamoto ya miundombinu hasa katika kipindi cha masika na kata ya kilimani Mtaa wa Chinyoyo ukiwa ni miongoni mwa changamoto ya miundombinu ya barabara za Mtaa huo.

“Sasa Mhe Diwani kutokana na upana mdogo wa miundombinu ya barabara za Mtaa wa Chinyoyo lazima tukae kwa pamoja ili tushee mawazo yetu kwa pamoja kwa kushirikiana na wataalamu juu ya kulipatia ufumbuzi swala hili ili tuondoe adha kwa wananchi”amesisitiza Mha.Mfinanga.

Awali akitoa taarifa ya changamoto ya Miundombinu ya barabara za kata ya kilimani Diwani wa kata ya kilimani Mussa Mkunda amesema katika kata yake mtaa ambao unafanya akose usingizi ni mtaa wa Chinyoyo kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara na ndio mtaa wenye wananchi wengi kuliko mitaa mingine ya kwenye kata yake.

“Hapa nikwambie tu Meneja mitaa inayo nifanya nikose usingizi ni huu mtaa wa Chinyoyo hasa katika kipindi hichi cha masika yani kila kukicha hodi haziishi nyumbani kwangu wananchi wanapishana tu kero kubwa ni barabara hivyo naomba mniangalie kwa jicho la tatu kuhakikisha tunaipatia ufumbuzi hii changamoto ya miundombinu ya barabara za Mtaa huu”alisisitiza Diwani Mussa Mkunda 

Aidha Mkunda amesema kutokana na uharibifu wa barabara hizo kunapelekea maji mengi kushuka katika mtaa wa Nyerere na kilimani na kwenda kuingia katika nyumba za mitaa hiyo na kufanya uharibifu mkubwa katika makazi wa watu wa mitaa hiyo.