March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‎Wanafunzi vyuo vikuu wapatiwa Mafunzo namna ya kuomba tenda za Serikali‎


‎Na Joyce Kasiki ,Timesmajira online,Dodoma

‎Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendesha mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na Mfumo wa NeST kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwaandaa vijana mapema kunufaika na fursa za ununuzi wa umma.

‎Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba, amesema mamlaka hiyo imejipanga kutembelea vyuo vikuu vyote nchini ili kutoa elimu kuhusu asilimia 30 ya fedha za zabuni zilizotengwa kwa makundi maalum, hatua itakayowawezesha vijana kuanza kujiandaa wakiwa vyuoni kuwa wajasiriamali na wamiliki wa makampuni watakaokuwa tayari kufanya kazi na serikali.

‎Amesema fursa hizo zinazotolewa na serikali zina uwezo wa kuwawezesha vijana kujenga makampuni makubwa na hata kuwa mabilionea endapo watazitumia kikamilifu.

‎Denis Simba ameongeza kuwa PPRA itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu nchini kwa kutoa mafunzo ya vitendo, kushiriki tafiti za kuboresha sera za ununuzi wa umma, pamoja na kujenga mazingira ya kidigitali ya kujifunzia Mfumo wa NeST ili wanafunzi waweze kuuelewa na kuutumia kwa vitendo.

‎Kwa mujibu wa PPRA, serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kujenga uwezo wa Watanzania kwa kutoa upendeleo wa asilimia 30 ya zabuni za kila taasisi ya umma kwa mwaka. Taasisi zote za umma zinatakiwa, katika mipango yao ya manunuzi, kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

‎Kwa upande wake, Gilbart Kamde, Meneja wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaonesha wanafunzi wa vyuo vikuu fursa zilizopo katika sekta ya ununuzi wa umma, huku yakilenga kubadili mtazamo wa vijana kutoka kuwaza kuajiriwa na badala yake kuwaza kuajiri wengine kupitia ujasiriamali.

‎Wakizungumza mara baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wanafunzi walioshiriki wamesema vijana wengi wamekuwa wakikata tamaa ya maisha kutokana na changamoto za ukosefu wa ajira, lakini kupitia mpango huu wa serikali wamepata matumaini mapya ya kujikwamua kiuchumi, kuanzisha biashara, na kuwa wafanyabiashara wakubwa watakaoshirikiana na serikali.