Na Mwandishi Wetu
KUANZIA Septemba 14, mwaka huu yanafanyika Maonesho ya One Stop Jawabu yanayoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yalianzia Viwanja vya Mbagala Zakhiem na sasa yanaendelea kwenye Viwanja vya Mwembe Yanga, ambapo yanatarajia kumalizika Septemba 28, mwaka huu.
Lengo la maonesho hayo ni kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi. Tangu kuanza kwa maonesho hayo mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, ambapo changamoto zao mbalimbali zimepatiwa ufumbuzi.
Ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi, taasisi mbalimbali za Serikali zinashiriki maonesho hayo. Miongoni mwa taasisi hizi ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Rebule Maira, anasema kupitia maonesho hayo Shirika linasikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama wake wanaofika katika banda lao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni mpango wa Serikali na shirika hilo wa kusogeza huduma karibu na wananchi.
Anasema katika kutekeleza majukumu manne ya Shirika, ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao, kupitia maonesho hayo NSSF inaandikisha wanachama wapya kutoka sekta rasmi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, mamalishe na bodaboda.
Pia, inatoa elimu mbalimbali kuhusu mafao yanayotolewa na Shirika hilo pamoja na kufanya uhakiki wa taarifa za wanachama wastaafu na wategemezi wao ili ziwekwe kwenye kumbukumbu sahihi.
“Kama munavyofahamu baada ya mabadiliko ya Sheria ya hifadhi ya jamii, sasa NSSF inahusika na watu waliopo katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi, hivyo kupitia maonesho haya tunahudumia makundi yote haya,” anasema.
Anasema kwa watumishi waliopo katika sekta rasmi wanaotembelea banda la Shirika hilo watapata nafasi ya kuangalia michango yao kama inapelekwa na mwajiri wake na kupata taarifa mbalimbali zinazohusu mafao na huduma nyengine zinazotolewa na NSSF.
Maira anasema NSSF imeweka lengo la kufikisha huduma zake kwa wananchi wote, na kwamba kwa wanachama wastaafu watapata fursa ya kuhakiki taarifa zao ambazo zitawekwa katika kumbukumbu sahihi za Shirika hilo ili waendelee kupokea mafao yao pasipo mkwamo wowote.
Anasema NSSF itaendelea kuwasaidia wananchi wa kawaida kwa kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kujiunga na Shirika hilo ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa yakiwemo ya urithi, uzazi na mirathi.
“NSSF inawaelimisha wananchi, inawaandikisha ili wananchi hawa wanufaike na huduma za hifadhi ya jamii,” anasema.
Meneja huyo wa NSSF amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) pamoja na benki ya Azania wataanza kutoa mikopo kwa wajasiariamali ili iwasaidie kuongeza mitaji yao.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliotembelea banda la NSSF kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali wametoa ushuhuda namna Shirika hilo linavyotatua changamoto zao ambazo kwa muda mrefu zilikosa majibu.
Mjane Kudra Mrisho Fumagwa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kupitia NSSF kwa namna inavyotatua changamoto zinazowakabili wananchi wa hali ya chini ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amejipambanua kuwatetea wanyonge.
“Naishukuru sana Serikali kupitia NSSF kwa namna inavyotatua changamoto hasa zinazotukabili sisi wajane na wananchi wote wa hali ya chini, siamini kama tatizo langu lingepatiwa ufumbuzi nasema asanteni sana NSSF,” amesema Kudra.
Anasema alikuwa anafuatilia madai ya mafao ya aliyekuwa mume wake, lakini baada ya kufika katika banda la NSSF shida yake imepatiwa ufumbuzi kwa haraka, na kwamba ameridhika na huduma zinazotolewa na Shirika hilo kwa wanachama wake.
Kudra amewaomba wananchi wenye shida mbalimbali kutembelea katika maonesho hayo ili waweze kupata ufumbuzi wa matatizo yao, huku akiwataka kupita kwenye banda la NSSF ili waweze kupata elimu na wajiunge na Shirika hilo kwa ajili ya kujiwekea akiba yao ya baadaye.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe ameipongeza NSSF kwa juhudi zake za kutatua kero zinazowakabili wanachama wake pamoja na kuwaelimisha wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi ili waweze kunufaika na hifadhi ya jamii baada ya kujiandikisha na Shirika hilo.
Kwa upande wake, Thomas Richard ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Kivulini Youth Network, amewaomba wenye vikundi kuwaandikisha wanachama wao NSSF ili wanufaike na huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo ikiwemo mafao na mikopo ya kukuza biashara zao.
“NSSF imeleta furaha katika kindi chetu, kwani katika yale mafao 7 yanayotolewa na Shirika hilo tumeanza kunufaika na mafao la matibabu,” anasema.
Amesema katika kupunguza gharama za maisha waliamua kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadae katika Shirika la NSSF, ambapo mpaka sasa wanachama 28 wa kikundi hicho wameshajiunga na Shirika hilo na wameanza kunufaika na mafao ya matibu.
Richard amesema wanachama wote wa kikundi hicho wameshuhudia wenyewe baada ya kujiunga na NSSF maisha yao yameanza kubadilika kwa sababu wananufaika moja kwa moja na mafao yanayotolewa na Shirika hilo.
“NSSF imeleta faraja kubwa katika kikundi chetu, imetuwezesha idadi ya wanachama kuongezeka hili ni jambo la kujivunia sana, tunaviomba vikundi vyengine wajiunge na Shirikaa hili,” anasema.
Naye mkazi wa Kibamba, Joseph Mihambo Raphael, ameishukuru NSSF kwa kupanua huduma zao na kuzisogeza karibu na wananchi na kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu ya hifadhi ya jamii pamoja na kujiunga na Shirika hilo.
Anasema baada ya kufika katika banda hilo alipatiwa huduma mzuri na tatizo lake limepatiwa ufumbuzi, ambapo aliwashauri wananchi na wanachama wa NSSF kutembelea banda hilo ili wanufaike na huduma mbalimbali zinazotolewa.
“Niwaombe wananchi na wanachama wa NSSF kutembelea banda la Shirika hili ili waweze kupata elimu na ufumbuzi wa changamoto zao,” anasema.
More Stories
Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika
CHADEMA wampongeza Mkurugenzi Mpanda
Ukosefu wa maji wasababisha wanafunzi kujisaidia vichakani