March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi za Elimu zaagizwa kuingiza  Mkakati wa kitaifa  katika Mipango yao

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amezitaka taasisi zote za elimu nchini kuingiza Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali na miongozo yake katika mipango yao ya taasisi, ili kufanikisha mageuzi ya kidijitali katika sekta ya elimu.

Prof. Nombo ameyasema hayo Leo Januari 14,2026 jijini Dodoma wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu na Miongozo yake, warsha inayofanyika Januari 14 na 15, 2026.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa mkakati huo unahitaji uongozi, uratibu madhubuti, rasilimali na uwajibikaji katika ngazi zote, akibainisha kuwa usambazaji wa mkakati na miongozo ni hatua ya kwanza tu, huku mkazo mkubwa sasa ukiwa ni utekelezaji.

“Mtakubaliana nami kwamba mabadiliko ya kidijitali si chaguo tena bali ni hitaji la lazima,kama inavyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ustawi wa baadaye wa Tanzania unategemea nguvu kazi yenye ujuzi wa kidijitali, ubunifu na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na soko la ajira,katika muktadha huu, elimu ndiyo msingi mkuu wa kufanikisha dira hiyo,” alisema Prof. Nombo.

Alieleza kuwa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali unaweka mfumo wa pamoja wa kitaifa wa kuratibu na kuongoza mageuzi ya kidijitali katika ngazi zote za elimu kuanzia shule za awali, msingi na sekondari, vyuo vya ualimu, elimu na mafunzo ya ufundi stadi (TVET), vyuo vikuu hadi ujifunzaji kupitia mifumo isiyo rasmi.

Prof. Nombo alisema mkazo wa sasa ni kwa kila mdau wa elimu kutafsiri mkakati huo kuwa vitendo vinavyoleta maboresho ya moja kwa moja katika ufundishaji, ujifunzaji, usimamizi na matokeo ya elimu kupitia matumizi bora ya teknolojia za kidijitali.

Kwa shule, vyuo vya ualimu, taasisi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) na vyuo vikuu, alibainisha kuwa utekelezaji unapaswa kuanza kwa kuimarisha misingi ya kidijitali ikiwemo upatikanaji wa intaneti, mitandao ya ndani, vifaa vya kidijitali, vyanzo vya umeme vya kuaminika pamoja na matumizi thabiti ya majukwaa ya kujifunzia mtandaoni na mifumo ya kidijitali iliyoidhinishwa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuingiza ujifunzaji mseto na ujifunzaji wa mtandaoni katika ufundishaji na tathmini za kawaida kwa kuhakikisha teknolojia inaongeza thamani na ufanisi bila kupunguza ubora wa ufundishaji.

Katika kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma, Prof. Nombo alihimiza taasisi kutoa kipaumbele kwa usawa na ujumuishaji, hasa kwa wanafunzi wa maeneo ya vijijini, wanafunzi wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

Akizungumzia nafasi ya walimu, Prof. Nombo amesema walimu na waelimishaji ndiyo nguzo kuu ya mageuzi ya kidijitali, akibainisha kuwa teknolojia pekee haiwezi kuleta mabadiliko ya kweli bila walimu wenye ujuzi na utayari wa kuitumia.

“Hivyo, vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na taasisi zote za mafunzo zinapaswa kujumuisha kwa makusudi ufundishaji wa kidijitali, ujumuishaji wa TEHAMA, uelewa wa Akili Unde (AI) pamoja na stadi za data katika programu za mafunzo ya awali na mafunzo kazini,” amesema Prof.Nombo

Ameongeza kuwa maendeleo endelevu ya kitaaluma (CPD) kupitia majukwaa ya kidijitali yanapaswa kuwa sehemu ya mfumo rasmi ili kuwawezesha walimu kutumia teknolojia kwa ubunifu, usalama na uwajibikaji.

Prof. Nombo pia amesisitiza umuhimu wa Miongozo ya Kitaifa ya Elimu ya Kidijitali pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Akili Unde (AI) katika Elimu, akieleza kuwa miongozo hiyo inaelekeza matumizi ya teknolojia na AI katika ufundishaji, utafiti, tathmini na utawala huku ikizingatia maadili, ulinzi wa data, uadilifu wa kitaaluma na ujumuishi.

Kuhusu utawala na udhibiti, amezihimiza taasisi za udhibiti na uthibitishaji ubora ikiwemo Tume ya vyuo vikuu (TCU), Baraza la Taifa na Elimu ya Ufundi (NACTVET),Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na ICTC kushirikiana kwa karibu ili kuoanisha viwango, kuimarisha uhakiki wa ubora na kuhakikisha miundombinu ya kidijitali inaendana na mahitaji ya ujifunzaji wa kidijitali, mseto na wa mtandaoni.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema warsha hiyo inalenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau na kuweka msingi wa utekelezaji wa mfumo mmoja wa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika ngazi zote za elimu nchini.

Amesema warsha hiyo inalenga kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu 2024/25–2029/30 pamoja na miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Shule na Vyuo vya Ualimu, Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Vyuo Vikuu pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Akili Unde katika Elimu.

Prof. Mushi ameongeza kuwa jitihada hizo zinaendana na mwelekeo wa taifa wa mabadiliko ya kidijitali na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika ngazi ya kikanda na kimataifa.