Na Penina Malundo,Timesmajira
Tume ya Bonde la Mto Nile (NBI),imempokea rasmi Mkurugenzi Mtendaji wake mpya wa 12,Dkt. Eng. Nestor Niyonzima,kutokea nchini Burundi ambaye ni Mkurugenzi wa pili kutoka Burundi kuongoza NBI.
Uteuzi Dkt.Eng Niyonzima ulithibitishwa na chombo cha juu zaidi cha uongozi cha NBI, Halmashauri ya Mawaziri wa Nile (Nile-COM),kwenye mkutano wao wa 33 uliofanyika Bujumbura, Burundi hivi karibuni.
Dkt. Eng. Niyonzima anachukua nafasi ya Dkt. Florence Grace Adongo wa Uganda, ambaye kipindi chake cha miaka miwili kama kiongozi wa tume kiliisha Desemba 2025.
Dkt. Callist Tindimugaya, ambaye aliwakilisha Uganda kwenye Kamati ya Ushauri wa Kiufundi (TAC) ya NBI, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji mpya na kusema anaanza kwa nguvu, akiongoza majadiliano muhimu kuhusu ushirikiano na uwekezaji wa kijamii na kiuchumi katika Bonde la Nile.
Dkt. Tindimunya akimuelezea Mkurugenzi wa NBI aliyemaliza muda wake alisema Dkt. Florence kuwa ni kiongozi mzuri,mwenye ushirikiano na mafanikio aliyoyashirikisha na vyombo vya uongozi na wadau wa NBI.

Akizungumzia uteuzi wake, Dkt. Eng. Niyonzima ameipongeza kamati hiyo iliyomteua kuongoza NBI na kudai kuwa ni hatua muhimu kwa mamilioni ya wananchi wa Bonde la Nile, ambao maisha yao yanategemea maamuzi wanayoyafanya na hatua mbalimbali wanazochukua.
Amesema anaanza kazi akiwa na misingi thabiti,pamoja na uwepo wa vipaumbele vyake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uaminifu na ushirikiano kati ya nchi wanachama, kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa NBI wa miaka 10, na kutoa matokeo yanayohusu wananchi.
Chini ya uongozi wa Dkt. Florence Grace Adongo, NBI ilipata mafanikio makubwa. Shirika hilo lilifanikiwa kushirikisha wadau wa kikanda, ikiwa ni pamoja na IGAD, Eastern Africa Power Pool na Tume ya Bonde la Ziwa Victoria, katika kukamilisha Mpango wa Uwekezaji wa Bonde la Mto Nile. Mpango huu unajumuisha miradi 59 ya kipekee inayolenga kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku ikipunguza uharibifu wa mazingira.
Aidha, NBI ilirejesha mfumo wa Kanda wa Ufuatiliaji wa Maji (Regional Hydrological Monitoring System), ambapo wataalamu wa kikanda sasa hufanya kazi kwa pamoja kubadilisha data za maji – wingi na ubora – kuwa taarifa za onyo mapema na ushauri kwa nchi wanachama kujiandaa na hali mbaya ya tabianchi. Mafanikio mengine ni pamoja na programu za mafunzo kwa vijana na jitihada za NBI kuanzisha Kituo cha Ubora cha Bonde la Nile, kikijenga msingi thabiti wa maarifa mtandaoni na mifumo 17 ya taarifa.
Dkt. Eng. Niyonzima, aliyezaliwa mwaka 1982, alipewa uteuzi na Serikali ya Burundi kuwa Waziri wa Mazingira, Kilimo na Mifugo, huku Calinie Mbarushimana, ndiye Mwenyekiti Mpya wa Nile-COM ambaye ana PhD ya Uhandisi wa Maji, shahada ya Uhandisi (Masters) katika Uhandisi wa Maji na Usimamizi wa Maji, pamoja na Diploma ya Kufundisha Chuo Kikuu kutoka Chuo Kikuu cha Moscow State University of Environmental Engineering, Urusi.
Kabla ya uteuzi wake, Dkt. Niyonzima ameshikilia nafasi mbalimbali za juu katika Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Burundi. Hivi karibuni alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Burundi na alikuwa kiongozi wa Mradi wa Sekta ya Maji na Kuimarisha Ustahimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi. Pia alifundisha kama mhadhiri wa juu katika Chuo Kikuu cha Burundi.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi