Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Longido
SERIKALI kupitia mradi wa maji wa Longido, imewezesha upatikanaji wa maji katika mji wa Longido na Kijiji cha Engikaret kwa asilimia 100, baada ya kukamilisha utekelezaji wa mradi wenye thamani ya sh. biloni 14.6, ambao unapokea maji kutoka chanzo cha Mto Simba ambao umekamilika Machi mwaka huu.
Akizungumza na wataalamu wa Wizara ya Maji waliopo katika ziara ya kukagua na kutathmini maendeleo ya miradi ya maji katika Mkoa wa Arusha, Mhandisi Salum Rasul kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi Arusha (AUWSA) amesema, mradi huo ni mkombozi kwa wakazi wa Longido na Kijiji cha Engikareti maeneo, ambayo yamekuwa na changamoto ya huduma ya maji safi na salama.
“Mradi umetekelezwa kwa lengo la kuongeza huduma ya maji kutoka asilimia 15 ambayo ilikuwa inawezesha wakazi 2,510 mwaka 2017 hadi asilimia 100, sawa na wakazi 16,712 waliopo sasa katika mji wa Longido pamoja na wakazi 1,294 wa Kijiji cha Engikaret.
Amesema, mradi huo umezingatia taratibu zote za afya, ikiwemo kuhakikisha maji hayo hayana madini ya floride yanayozidi kiwango.
Rasul amesema, hiyo ni hatua nzuri kwa maendeleo ya wananchi wa Longido na Mkoa wa Arusha kwa ujumla.
Naye Mkuu wa msafara wa wataalamu waliotoka Wizara ya Maji, Ingrid Sanda alisema serikali imejipanga kuhakikisha inamtua mama ndoo ya maji kama ilivyoahidi, huku akiwataka wakazi wa maeneo hayo kuhakikisha wanailinda miundombinu ya maji ili isiharibike.
Kwa upande wake, Anna Revocatus ambaye ni mkazi wa Longido amesema maji hayo yamewawezesha kubadili maisha yao kwa kuanzisha kilimo cha bustani na kuwezesha mazingira ya kupendeza.
Mwananchi mwingine, Abel Kundaeli amesema ameanzisha shamba la vitunguu na matarajio yake ni kuuza ndani na nje ya nchi, ambapo kwa sasa shamba hilo limetoa ajira kwa watu 10 na anatarajia kupanua zaidi.
Kuhusu gharama za maji, Kundaeli amesema ni nafuu ikilinganishwa na soko la bidhaa za kilimo katika miji ya Arusha na nchi jirani ya Kenya.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia