Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya
WATAALAMU wa Benki ya NMB wametakiwa kuendelea kutoa elimu ya fedha, uwekezaji na ujasiriamali kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kuboresha maisha yao pamoja na wananchi wanaotumia huduma za benki hiyo.
Wito huo umetolewa Januari 7 ,2026, na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, wakati wa ziara ya maofisa wa Benki ya NMB hospitalini hapo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili.

Dkt. Mbwanji ameipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii pamoja na kushirikiana vyema na hospitali hiyo katika masuala ya kifedha kwa watumishi wake. Ameeleza kuridhishwa na namna benki hiyo inavyoshirikiana na hospitali katika kutoa huduma mbalimbali, hususan kwa watumishi.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kuendeleza ushirikiano uliopo, kujadili masuala ya huduma za kifedha, pamoja na kuboresha maendeleo ya mtu mmoja mmoja kifedha.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa Benki ya NMB Makao Makuu, Hellen Lema, amepongeza uongozi na watumishi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa kutoa huduma za kibingwa na bobezi kwa Watanzania pamoja na watumishi wa benki hiyo. Pia ameipongeza hospitali kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya kisasa ya kutolea huduma.

“Tunawapongeza sana kwa jitihada zenu kubwa mnazofanya katika tiba bobezi ,lakini upande wa miundombinu ya kisasa mmefanya kazi kubwa sanaa”amesema .Lema.
Bi. Lema amesema Benki ya NMB inajivunia kuwa na hospitali hiyo kama mshirika muhimu katika kutoa huduma kwa watumishi na taasisi, na kuahidi kuendeleza mahusiano hayo mazuri kwa manufaa ya pande zote.
Ugeni huo wa Benki ya NMB Makao Makuu Dar es Salaam umeongozwa na Afisa Uhusiano, Bi. Hellen Lema, akishirikiana na Ndugu Angumbwike Ngogo kutoka Tawi la Mwanjelwa, Mbeya.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi