*Wananchi wahimizwa kujitokeza katika upimaji huo
Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online-Dar
WANANCHI wa Kata ya Kilakala Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar-es-Salaam wameombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la upimaji wa mabusha linaloendelea katika zahanati ya Kilakala ili waweze kupata matibabu bure.
Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Kilakala, Erick Zuberi wakati akizugumza na waandishi wa habari ambapo amesema zoezi hilo lilianza Januari 5 na linatarajiwa kukamilika Januari 30,2026,ikiwa ni sehemu ya operesheni maalumu ya upasuaji wa mabusha inayoratibiwa na Wizara husika.
“Tumepewa bahati katika Wilaya yetu ya Temeke, hususani zahanati ya Kilakala, kupata huduma ya operesheni ya mabusha bure kutoka wizarani,wananchi wanaendelea kujiandikisha na wale watakaobainika watafanyiwa upasuaji kuanzia siku ya Ijumaa,”amesema Zuberi.
Ameongeza kuwa mwitikio wa wananchi ni mzuri, huku akibainisha kuwa hadi sasa watu 75 wamejiandikisha na kufanyiwa vipimo, na zaidi ya wananchi 50 tayari wamekamilisha taratibu za awali kuelekea kufanyiwa upasuaji.
“Huduma hii ni bure kabisa, hivyo tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kabla ya zoezi kufikia tamati,” amesema.
Amesema hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ikiwemo masuala ya bima ya afya na huduma muhimu za kijamii.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi