Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kugusa maisha ya wananchi kwa vitendo,
baada ya kuendesha kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya macho.
Kambi hiyo wakishirikiana na Taasisi ya Bilal Muslim Mission jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kusaidia jamii unaoendelea kutekelezwa kote nchini.
Akifanya mahojiano na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kati, Said Idd amesema mbali na kutoa huduma za mawasiliano, Yas imejikita pia kutoa huduma zinazolenga kuboresha ustawi wa wananchi, hususan wenye kipato cha kawaida.
“Mbali na kutoa huduma za mawasiliano, leo tumeamua kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa kutoa huduma za afya ya macho.
“Hii inasaidia kupunguza changamoto za kiuchumi kwa wananchi ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu,” amesema Idd.
Idd ameongeza kuwa, hii si mara ya kwanza kwa Yas kuendesha huduma hizo, kwani kampuni imekuwa ikifanya kambi za matibabu ya macho katika maeneo mbalimbali nchini tangu mwaka 2024, na kufanikiwa kuwahudumia zaidi ya wagonjwa 35,000.
Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Kambi za Macho kutoka Bilal Muslim Mission, Hassan Dinya amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali, Yas na wadau wengine wa afya.
“Katika siku ya leo pekee tumefanikiwa kupokea na kuhudumia takribani wananchi 600. Huu ni uthibitisho kuwa huduma hizi bado zinahitajika kwa kiwango kikubwa,” amesema Dinya.
Wananchi wa jiji la Dodoma waliohudumiwa katika kambi hiyo walitoa shukrani kwa Serikali na Yas kwa kuwajali wananchi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya macho.
Walisema, huduma hiyo imewasaidia kugundua matatizo ya macho mapema na kupata matibabu sahihi.
Aidha, wananchi walitoa wito kwa kambi kama hizi kuendelea kufanyika mara kwa mara na kufikishwa hadi maeneo ya vijijini ili kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani