Na Esther Macha ,TimesmajiraOnline, Mbeya
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amemtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi wa bweni la wasichana katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole, Jijini Mbeya, kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuendana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa kike.
Mahundi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni hayo, ambao umefikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji.

Pia amehimiza uwajibikaji, usimamizi madhubuti na matumizi sahihi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo.
“Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni tano katika ujenzi wa bweni hili. Ni wajibu wa mkandarasi, msimamizi wa mradi na uongozi wa Chuo kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na mradi huu unakamilika kwa ubora na kwa wakati,” amesema Mhandisi Mahundi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Mbeya, Edina Mwaigomole, amesema ujenzi wa bweni hilo ni hatua muhimu katika kumlinda na kumwezesha mtoto wa kike kielimu, hususan wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.
“Bweni hili ni suluhisho la changamoto nyingi zilizokuwa zinawakabili wasichana, ikiwemo ukosefu wa makazi salama. UWT tunaipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowasaidia wasichana kusoma kwa utulivu na kujiendeleza,” amesema Edina.
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole, Silvester Mwambene, amesema kukamilika kwa mabweni hayo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike pamoja na kupunguza changamoto za kijamii zilizokuwepo awali.

“Mabweni haya yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 600. Yatasaidia kuondoa changamoto ya makazi na kupunguza hatari za mimba zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike kwa kuwapatia mazingira salama na rafiki kwa masomo,” amesema Mwambene.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa mabweni hayo, Latoi Mollel, amesema maandalizi ya mwisho yanaendelea na mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi